Uvamizi Laikipia: Mbunge wa zamani Lempurkel atiwa mbaroni

Muhtasari

• Wafuasi wake walianza kukusanyika nje ya ofisi za DCI za Nairobi baada ya kupata habari kwamba alikuwa huko.

• Jumanne, kamishna wa kanda ya Bonde la Ufa George Natembeya alidai kuwa baadhi ya wavamizi hao walikuwa na silaha za kisasa kuliko polisi.

Mbunge wa zamani wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel Picha: STAR
Mbunge wa zamani wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel Picha: STAR

Mbunge wa zamani wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel amekamatwa kutoka nyumbani kwake mtaani Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado kutokana na mapigano yanayoendelea Laikipia.

Baadaye alihamishiwa eneo la DCI Nairobi kuhojiwa na huenda akapelekwa kuzuiliwa mahali pengine kama vile Nakuru au Nanyuki.

Haijulikani ni kwa nini anahusishwa na mapigano huko Laikipia lakini polisi walisema alikuwa mtu wa maana katika uchunguzi wao na ataruhusiwa kuzungumza na wanahabari baadaye.

Wafuasi wake walianza kukusanyika nje ya ofisi za DCI za Nairobi baada ya kupata habari kwamba alikuwa huko.

Sio mara ya kwanza kwa mbunge huyo wa zamani kushikwa kuhusiana na machafuko katika eneo hilo.

Hivi sasa anakabiliwa na mashtaka mahakamani kuhusiana na machafuko ya zamani katika eneo hilo.

Kukamatwa kwake kunajiri wakati serikali inaendeleza operesheni kali ya usalama katika eneo la Laikipia Nature Conservancy ikilenga wafugaji waliojihami na ambao wameteka eneo hilo na kufurusha wenyeji.

Jumanne, kamishna wa kanda ya Bonde la Ufa George Natembeya alidai kuwa baadhi ya wavamizi hao walikuwa na silaha za kisasa kuliko polisi.

"Wakati maafisa wetu wakitumia bunduki za AK 47 na G3, majangili wanatumia M16 na bunduki zingine nzito ambazo kawaida hutumiwa na majeshi ya kigeni," alisema.

"Hatujui ni vipi wanapata silaha hizi nzito."