Mfumo wa elimu wa CBC utaendelea nchini licha ya kushtumiwa vikali

Muhtasari

•Hatua hiyo inawadia baada ya washikadau mbalimbali wa elimu kuibua wasiwasi juu ya mtaala huo wa CBC, wakisema ni ghali mno kwa wazazi, vifaa vinavyohitajika kuutekeleza kikamilifu havipatikani kwa urahisi, unachukua muda mwingi wa wazazi na malalamishi mengineo.

CS magoha
CS magoha

Waziri wa Elimu nchini Kenya, Profesa George Magoha, ametupilia mbali shutuma za wale wanaokosoa utekelezaji wa Mtaala mpya wa elimu nchini humo (CBC), akisema utekelezaji wake utaendelea kama ilivyopangwa.

Hatua hiyo inawadia baada ya washikadau mbalimbali wa elimu kuibua wasiwasi juu ya mtaala huo wa CBC, wakisema ni ghali mno kwa wazazi, vifaa vinavyohitajika kuutekeleza kikamilifu havipatikani kwa urahisi, unachukua muda mwingi wa wazazi na malalamishi mengineo.

Akizungumza wakati akihitimisha zoezi la kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021 chini ya sera mpya inayohitaji watoto wote waliofanya mtihani kujiunga na shule za upili, Profesa Magoha alisema serikali imejitolea kuhakikisha mtaala wa CBC unatekelezwa kikamilifu.

Bwana Magoha alisema kuwa ukosoaji uliopo umeingizwa siasa ndani yake na kuahidi kwamba wao sio wanasiasa wala waoga.

‘’Hamutaniona kwenye televisheni nikibishana lakini nitakuwa shuleni nikihakikisha kuwa kazi inaendelea. Na ikiwa kuna changamoto zozote tutazishughulikia,” alisema.

Waziri Magoha aliahidi kuwa serikali imeweka mikakati ya kununua vifaa vyautekelezaji wa mtaala huo na kupuuza madai kwamba vitabu vya kiada vinavyohitajika ni ghali mno kwa wazazi.

Mtaala wa CBC wa mfumo wa 2-6-3-3-3 ambao ulianzishwa mnamo mwaka 2017 kuchukua nafasi ya mfumo wa elimu wa 8-4-4 bado haujakubaliwa kabisa na wahusika wote.

Wakati huohuo, Rais wa Chama cha wanasheria nchini Kenya (LSK) Nelson Havi, amevunja ukimpya na kutangaza mipango ya kupinga mtaala mpya mahakamani.

Havi anasema kuwa mfumo mpya wa elimu nchini Kenya haupaswi kuwa ghali, na jaribio lisilofaa kwa watoto na maisha yao ya baadaye kama ilivyo kwa uongozi.

Aidha, raia chini Kenya wamekuwa wakitoa hasira zao kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha vile mfumo huo mpya wa elimu umekuwa kama mzigo kwao.