Ujenzi wa nyumba zilizotekezwa Laikipia wang'oa nanga huku makao mapya ya polisi yakijengwa

Muhtasari

•Wahasiriwa wanaendelea kupokea msaada wa chakula  na vifaa vya ujenzi huku wakipongeza hatua ambazo serikali imechukua kukabiliana na ukosefu wa usalama maeneo hayo

•Shule ambazo zilikuwa zimefungwa kufuatia ghasia zinatarajiwa kufungulia tena siku ya Jumatatu huku Matiang'i akiagiza polisi kuandamana na walimu na wanafunzi wanapoenda shuleni katika eneo la Ol-Moran.

Nyumba zilizotekezwa katika kijiji cha Kisii Ndogo
Nyumba zilizotekezwa katika kijiji cha Kisii Ndogo
Image: ELIUD WAITHAKA

Hatua ya kujenga upya manyumba ambayo yaliteketezwa na wavamizi katika kaunti ya Laikipia imeng'oa nanga.

Kupia ujumbe uliotolewa wanahabari siku ya Jumamosi, wizara ya masuala ya ndani na uratibu wa kazi za serikali ambayo inaongozwa na waziri Fred Matiang'i imesema kuwa hali ya utulivu inarejea polepole katika kaunti hiyo.

Wahasiriwa wanaendelea kupokea msaada wa chakula  na vifaa vya ujenzi huku wakipongeza hatua ambazo serikali imechukua kukabiliana na ukosefu wa usalama maeneo hayo.

Siku ya Ijumaa waziri Matiang'i alizindua ujenzi wa makao makuu mapya ya polisi katika eneo la Ol-Moran kufuatia kuongezwa kwa maafisa wa usalama katika maeneo hayo.

"Tumeongeza idadi ya maafisa hapa na tumeanza ujenzi wa makao makuu ya polisi  katika eneo la Ol-Moran. Kituo hicho kitakuwa na maafisa zaidi ya mia moja" Alisema Matiang'i alipokuwa anazindua rasmi ujenzi wa kituo hicho.

Matiang'i ambaye alikuwa ameandamana na naibu inspekta wa polisi Noor Gabow, kamanda wa polisi katika eneo la bonde la Ufa George Natembeya na gavana wa Laikipia Nderitu Muriithi alisema kuwa kuongezwa kwa maafisa na ujenzi wa vituo viwili vya polisi zitasaidia kulinda wakazi dhidi ya majambazi.

Mradi wa kujenga makao mapya ya polisi utasimamiwa na serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti ya Nakuru. Kupitia serikali yake, gavana Muriithi ametoa shilingi milioni 20 kusaidia mradi huo.

Shule ambazo zilikuwa zimefungwa kufuatia ghasia zinatarajiwa kufungulia tena siku ya Jumatatu huku Matiang'i akiagiza polisi kuandamana na walimu na wanafunzi wanapoenda shuleni katika eneo la Ol-Moran.