Mikutano ya hadhara yapigwa marufuku katika kaunti ya Laikipia kufuatia ghasia

Muhtasari

•Mikutano ya kisiasa haipaswi kufanyika pale kwani tayari imetangazwa kuwa hilo ni eneo lililofadhaika na kuna operesheni ya usalama inayoendelea.

•Matiang'i alisema kuwa hali ya utulivu imeanza kurejea pale huku makao mapya ya polisi yakiendelea kujengwa kufuatia kuongezwa kwa maafisa wa usalama upande huo.

Mutyambai
IG Hillary Mutyambai Mutyambai

Ofisi ya Inspekta Jenerali wa polisi imepiga marufuku mikutano ya hadhara kufanyika katika kaunti ya Laikipia ambayo imekabiliwa na ghasia siku za hivi karibuni.

Kupitia ujumbe uliotolewa  na idara ya polisi kwa waandishi wa habari siku ya Jumamosi, mikutano ya kisiasa haipaswi kufanyika pale kwani tayari imetangazwa kuwa hilo ni eneo lililofadhaika na kuna operesheni ya usalama inayoendelea.

Ujumbe huo ambao umetiwa saini na mkurugenzi wa mawasiliano katika idara ya polisi Bruno Shioso unasema kuwa hatua kali itachukuliwa dhidi ya mtu ama kikundi cha watu ambacho kitakaidi agizo hilo .

"Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanapanga kufanya mikutano hata katika maeneo  ya kaunti ya Laikipia ambayo yametangazwa kwa gazeti la kitaifa kuwa yanafadhaika.

Idara ya polisi ingetaka kuwakumbusha kuwa maeneo hayo yametangazwa kufadhaika huku kukiwa na operesheni ya usalama ambayo inaendelea. Itabaki kuwa hivyo hadi tangazo hilo litakapofutwa.

Kwa hivyo ni haramu na utowajibikaji kufanya mikutano ya umma kwa kukiuka sheria. Hatua itachukuliwa dhidi ya eyote ama kikundi cha watu kitakachokaidi agizo hilo" Ujumbe huo ulisoma.

Waziri Matiang'i amesema kuwa ujenzi wa nyumba ambazo zileteketezwa katika eneo hilo wakati wa ghasia umeanza.

Matiang'i alisema kuwa hali ya utulivu imeanza kurejea pale huku makao mapya ya polisi yakiendelea kujengwa kufuatia kuongezwa kwa maafisa wa usalama upande huo.