Shule zafunguliwa Laikipia huku usalama ukiendelea kuboreshwa

Muhtasari

•Maafisa zaidi wameongezewa katika maeneo hayo ili kuboresha usalama na kuwafurusha majambazi ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi.

• Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai amehakikishia wananchi kuwa hali ya kawaida imerejea katika maeneo yaliyokuwa yameathirika akidai kuwa majambazi wameweza kufurushwa pale

Polisi walinda shule Laikipia
Polisi walinda shule Laikipia
Image: NPS

Shule zimefunguliwa asubuhi ya Jumatatu katika maeneo mbalimbali ya kaunti ya Laikipia ambayo yalikuwa yamekabiliwa na ghasia siku za hivi karibuni.

Maafisa zaidi wameongezewa katika maeneo hayo ili kuboresha usalama na kuwafurusha majambazi ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi.

Huku wanafunzi wengi wakirejea polisi wameonekana wakilinda shule hizo ili kuwapa watoto hao usalama.

Alipokuwa kwenye ziara yake maeneo hayo wiki iliyopita  waziri Fred Matiang'i aliagiza shule zifunguliwe leo (Jumatatu) na kuelekeza maafisa wa usalama kuwapa wanafunzi pamoja na waalimu usalama.

Matiang'i alisema kwamba hali ya utulivu ilikuwa inarejea katika kaunti hiyo huku nyumba zilizokuwa zimeteketezwa zikianza kujengwa upya.

Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye ukurasa wake wa Twitter, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai amehakikishia wananchi kuwa hali ya kawaida imerejea katika maeneo yaliyokuwa yameathirika akidai kuwa majambazi wameweza kufurushwa pale.

"Majambazi wameondolewa na kikosi cha maafisa wa usalama. Hali ya kawaida imerejea katika maeneo yaliyoathiriwa.. Tunaendelea kushirikiana na jamii, viongozi pamoja na washika dau wengine na kuwashawishi wajihusishe na mipango ya usalama" Mutyambai amesema.

Siku ya Jumamosi Mutyambai alitoa ujumbe kwa waandishi wa habari akitangaza kupigwa  marufuku kwa mikutano ya hadhara katika kaunti ya Laikipia