Seneta wa zamani Chris Obure ana kesi ya kujibu kuhusiana na sakata ya Anglo leasing iliyohusisha Sh928M- Mahakama

Muhtasari

•Hakimu Anne Mwangi ameagiza Obure pamoja na wengine waliokuwa maafisa wa serikali kujitetea akisema kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi yao

Image: FACEBOOK// CHRIS OBURE

Habari na Susan Muhindi

Mahakama ya kupambana na ufisadi imempata aliyekuwa seneta wa Kisii Chris Obure na kesi ya kujibu kwenye kesi ya sakata ya Anglo leasing iliyohusisha shilingi milioni 928.

Hakimu Anne Mwangi ameagiza Obure pamoja na wengine waliokuwa maafisa wa serikali kujitetea akisema kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi yao.

"Baada ya kuangazia ushahidi ambao umetolewa naona kwamba serikali iko na kesi wazi  dhidi ya washtakiwa" Bi Mwangi alisema.

Kwenye kesi hiyo, Obure ambaye kwa sasa ni katibu mkuu wa  utawala katika wizara ya uchukuzi ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa PS katika wizara ya mawasiliano  Samuel Kyungu, Samuel Bundotich na marehemu Francis Chahonyo.

Wanne hao walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya serikali juu ya kandarasi iliyotiwa saini mwaka wa 2003 kati ya serikali na kampuni tatu za kusambaza huduma za mitandao.

Kandarasi hiyo ambayo Obure anadaiwa kuidhinisha itiwe saini ilkuwa na thamani ya dola milioni 11.8(Shilingi 928M).

Hakimu aliagiza kesi hiyo itajwe tena mnamo tarehe 8 Oktoba ambapo washtakiwa watasema namna wangependa kujitetea