Jamaa matatani baada ya mti ambao alikuwa analenga kugonga mkewe nao kupata bintiye na kumuua

Muhtasari

•Amos Maengwe (30) alikuwa anapigana na mkewe Esther Kaiseyi  (21) nyumbani kwao katika mtaa wa Majengo, mji wa Kilgoris wakati alichukua kipande cha mti na kujaribu kumgonga nacho ila akamkosa na kupata bintiye.

•Kwa bahati mbaya mtoto yule alifariki alipokuwa anahudumiwa na madaktari kwani hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya zaidi.

crime scene 1
crime scene 1

Msichana wa miaka nane alipoteza maisha yake usiku wa Jumatatu baada ya babake kumgonga kwa kipande cha mti walipokuwa wanazozana na mamaye.

Amos Maengwe (30) alikuwa anapigana na mkewe Esther Kaiseyi  (21) nyumbani kwao katika mtaa wa Majengo, mji wa Kilgoris wakati alichukua kipande cha mti na kujaribu kumgonga nacho ila akamkosa na kupata bintiye.

Baada ya tukio hilo ambalo halikuwa limekisiwa kutokea wapenzi hao wawili walisitisha vita yao na kuanza juhudi za kunusuru maisha ya binti yao ambaye alikuwa anabubujikwa na damu tiriri.

Kulingana na DCI, Maengwe na Kaiseyi walimchukua mtoto huyo na kuanza safari ya kumpeleka katika hospitali iliyokuwa karibu wakiwa na matumaini ya kuokoa maisha ya binti yao.

Walipokuwa njiani kuelekea hospitalini walikutana na maafisa wa polisi ambao waliwasimamisha na kuwahoji kisha kuwasaidia kukimbiza mhasiriwa hadi hospitali ya kaunti ndogo ya Kilgoris baada ya kuona hali yake.

Kwa bahati mbaya mtoto yule alifariki alipokuwa anahudumiwa na madaktari kwani hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya zaidi.

Papo hapo wazazi wa marehemu walitiwa pingu na kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilgoris huku uchunguzi zaidi ukiendelea.