Serikali ya Kenya yatangaza msako dhidi ya wahamiaji haramu

Muhtasari

•Takwimu iliyotolewa na wizara mambo ya ndani zinaonesha kuwa zaidi ya raia wa kigeni 20,000 wameinga nchini tangu mwezi Juni. Karibu 8,000 kati yao wameondoka.

Image: BBC

Serikali ya Kenya imetangaza msako dhidi ya raia wa kigeni walio nchini humo kiharamu.

Hii ni baada ya hofu kuzuka juu ya ongezeko la makundi ya raia wa kigeni- wengi wao kutoka bara Asia ambao wameonekana katika maeneo ya makazi jijini Nairobi.

Takwimu iliyotolewa na wizara mambo ya ndani zinaonesha kuwa zaidi ya raia wa kigeni 20,000 wameinga nchini tangu mwezi Juni. Karibu 8,000 kati yao wameondoka.

Katibu katika Wizara ya Mambo ya ndani, Karanja Kibicho, alisema wageni hao wako njiani kuelekea Saudi Arabia kwa kazi.

Saudi Arabia imejumuisha nchi kadhaa za Asia katika orodha nyekundu, ambayo ilibuniwa kuzuia kusambazwa kwa virusi vya corona.

Bw. Kibicho hata hivyo amesema Kenya inakabiliwa na tishio la kuenea zaidi kwa virusi vya Covid-19 ndiposa inataka kudhibiti idadi ya watu wanaopita nchini hiyo.

Raia hao wa kigeni wanaishi Nairobi na jimbo jirani la Machakos.

Vyama vya wakaazi vimekuwa vikihoji ikiwa wageni hao wanazingatia kanuni zilizowekwa za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kama vile kuvaa barakoa.