"Inasikitisha" Rais Kenyatta aomboleza kifo cha wakili wake Evans Monari

Muhtasari

•Rais Kenyatta alimtaja Monari kama wakili wa kutegemewa ambaye ameacha urithi mkubwa wa mafanikio kwenye taaluma yake.

•Monari pia aliwakilisha aliyekuwa kamishna wa polisi Hussein Ali na Francis Muthaura wakati walishtakiwa katika mahakama ya Hague kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Marehemu Evans Monari
Marehemu Evans Monari
Image: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta ameomboleza kifo cha wakili Evans Monari ambaye alifariki katika hospitali ya Nairobi usiku wa Jumatatu baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

Rais Kenyatta alimtaja Monari kama wakili wa kutegemewa ambaye ameacha urithi mkubwa wa mafanikio kwenye taaluma yake.

"Inasikitisha kuona kuwa tumepoteza Evans kwa mkono katili wa kifo kufuatia maradhi ya kipindi kirefu. Alikuwa miongoni mwa mawakili bora nchini aliyejitambulisha kama mtu wa kutegemewa kama mafanikio yake yalivyoonyesha" Rais alisema.

Monari ambaye alikuwa miongoni mwa mawakili ambao waliwakilisha rais Kenyatta amekuwa akilazwa hospitalini mara kwa mara kutokana na maradhi ambayo yamemwathiri kwa kipindi kirefu. Kufikia kifo chake alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Alikuwa mmiliki mwenza wa kampuni ya sheria ya Bowman jjjini Nairobi ana alikuwa na utaalam mkubwa katika masuala ya kibiashara, umma, uhalifu katiba na malalamishi kwenye chaguzi.

Monari pia aliwakilisha aliyekuwa kamishna wa polisi Hussein Ali na Francis Muthaura wakati walishtakiwa katika mahakama ya Hague kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Rais Kenyatta alifariji familia ya marehemu na kuwaombea faraja ya Mola wanapokabiliana na kuaga  kwa mpendwa wao.