Chanjo ya Malaria: Wadau wakaribisha kuidhinishwa kwa chanjo

Muhtasari

• Kulingana na data ya Unicef, mtoto mmoja hufa kila dakika mbili kutokana na malaria.

Wadau katika sekta ya afya wamepongeza idhinisho la shirika la afya duniani WHO la matumizi mapana ya chanjo ya kwanza ya malaria ulimwenguni -RTS, S / AS01E (RTS, S) - ambayo jina lake la biashara ni Mosquirix.

"Inafurahisha kujua kwamba chanjo ya malaria iliyotengenezwa mahususi kwa watoto wa Kiafrika hivi karibuni inaweza kupatikana zaidi," Mkuu wa shirika la PATH wa Kanda ya Afrika Dkt Nanthalile Mugala alisema katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano.

"Hii ni kweli sasa, wakati maendeleo katika kupambana na malaria yamekwama katika sehemu za eneo la Afrika na watoto wanabaki katika hatari kubwa ya kufa kutokana na ugonjwa huo."

PATH imeshughulika na ukuzaji na utekelezaji wa chanjo hiyo kwa zaidi ya miaka 20.

"Wakati walezi walipoona faida za chanjo ya malaria kwa watoto wao, tuliona imani yao kwa chanjo, na mifumo ya afya inakua," alibainisha Dk Mugala.

Kulingana na data ya Unicef, mtoto mmoja hufa kila dakika mbili kutokana na malaria.

Mkuu wa idara ya mpango wa Malaria Dkt George Githuka alisema watoto 220,000 walifaidika na mpango wa majaribio na walipatiwa chanjo.

"Majaribio ya kwanza yalilenga kuona ikiwa chanjo hiyo itakubaliwa na athari itakayokuwa nayo katika suala la kupunguzwa kwa visa vya malaria," alisema wakati wa mahojiano na Star.

"Akina mama walikuwa na matumaini kuhusu chanjo hiyo na ilipewa watoto, pamoja na chanjo zingine na haikuwaathiri."

"Huyu ni mwanzo mpya na mchango wake utaonekana baadaye."

Kupitia mipango inayoendelea ya majaribio nchini Ghana, Malawi na Kenya, zaidi ya watoto 800,000 wamefikiwa kwa zaidi ya miaka mitatu tangu 2019.

Imeonekana kuwa nzuri, ikiwa imejaribiwa kupitia chanjo ya kawaida ya watoto katika maeneo yaliyoathiriwa nchini kama vile Kisumu, Busia na Kakamega ambapo iliripotiwa kwamba theluthi mbili ya watoto ambao hawakuwa wakilala chini ya vyandarua vya kuzuia mbu.