Jamaa ashambulia mkewe, mama mkwe na jirani kwa kisu baada ya kuzuiwa kuona wanawe Laikipia

Muhtasari

•Inasemekana kwamba Mwaura alikusudia kuchukua watoto wake kutoka kwa mkewe  Susan Wairimu  ambaye amekuwa akiishi nao tangu watengane  miezi miwili iliyopita.

•Mwaura anadaiwa kutoa kisu na kushambulia mama mkwe akiwa na nia ya kumdunga. Mkewe kuona hivo akakimbia kumkinga mama yake dhidi ya mumewe na akajeruhiwa pia.

Crime scene
Crime scene

Polisi katika kaunti ya Laikipia wanazuilia jamaa mmoja anayetuhumiwa kushambulia mkewe, mama mkwe na jirani yao katika eneo la Marmanet kufuatia mzozo uliohusisha watoto.

Chistopher Mwaura ambaye alikuwa amesafiri kutoka jijina Nairobi hadi eneo la Maili Saba kaunti ya Laikipia anaripotiwa kushambulia watatu hao kwa kisu baada ya kukatazwa kuona watoto wake.

 Inasemekana kwamba Mwaura alikusudia kuchukua watoto wake kutoka kwa mkewe  Susan Wairimu  ambaye amekuwa akiishi nao tangu watengane  miezi miwili iliyopita.

Mama mkwe alijaribu kumshirikisha Mwaura kwenye mazungumzo ili maafikiano mazuri yapatikane ila juhudi zake zikagonga mwamba mna mzozo mkubwa ukaibuka kati yao.

Mwaura anadaiwa kutoa kisu na kushambulia mama mkwe akiwa na nia ya kumdunga. Mkewe kuona hivo akakimbia kumkinga mama yake dhidi ya mumewe na akajeruhiwa pia.

Jirani  mmoja aliyetambulishwa kama Paul Gichuki alijaribu kuingilia kati ili kuokoa Bi. Wairimu ila akadungwa kwenye ubavu katika hekaheka zile.

Watatu hao walipelekwa katika hospitali ya Nyahururu ambako walipokea matibabu huku mshukiwa akitiwa mbaroni na kusubiri kushtakiwa.