Rais Kenyatta amuomboleza mtangazaji mkongwe Badi Mukhsin

Muhtasari

•Kenyatta amemtaja marehemu kama  mtangazaji aliyekuwa na talanta kubwa na kielelezo bora kwa watangazaji chipukizi.

•Kenyatta alisema kwamba wengi walipendezwa na ufasaha wa Mukhsin wa lugha ya Kiswahili na utulivu wake alipokuwa anasoma habari. 

Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ameungana na Wakenya wengine kumuomboleza mtangazaji mkongwe wa KBC Badi Mukhsin ambaye alifariki siku ya Ijumaa akiwa mjini Mombasa.

Kenyatta amemtaja marehemu kama  mtangazaji aliyekuwa na talanta kubwa na kielelezo bora kwa watangazaji chipukizi.

Kulingana na rais Kenyatta, marehemu Badi alikuwa mtangazaji mwaminifu ambaye alikuwa amejitolea kabisa  kwenye taaluma yake ya utangazaji.

"Alikuwa mwaminifu kabisa, thabiti na akijitolea kabisa kwenye taaluma yake na mwajiri wake KBC. Muhsin alikuwa mwanzilishi wa kikweli nchini Kenya na kielelezo kizuri. Kurejea kwake KBC baada ya miaka mingi kuliashiria kitendo cha kujitolea na upendo mkubwa kwa taaluma na nchin yake" Rais Kenyatta aliomboleza.

Kenyatta alisema kwamba wengi walipendezwa na ufasaha wa Mukhsin wa lugha ya Kiswahili na utulivu wake alipokuwa anasoma habari. 

Alisema kuwa mtangazaji huyo atapezwa milele kwenye runinga zetu kutokana na umahiri ambao alionyesha katika kazi yake.

"Wakenya wengi walifurahia utulivu wake alipokuwa anatangaza, Kiswahili chake kizuri na uwepo wake. tindo wake wa kipekee ulipendwa na wengi ambao watampeza milele" Alisema rais.

Kenyatta alifariji familia ya marehemu pamoja na marafiki na mashabiki huku akiomba Mola awajalie nguvu za kupambana na majonzi.