"Mimi ni mzima!" Familia ya Charles Njonjo yapuuzilia mbali uvumi kuwa amefariki

Muhtasari

•Ujumbe ambao ulitolewa na familia yake kwa vyombo vya habari umethibitisha kwa Njonjo ako salama salimini na anafurahia wikendi akiwa nyumbani kwake.

•Uvumi kuhusu kifo cha mkongwe huyo wa miaka 101 ulienezwa sana mitandaoni siku ya Jumamosi

Image: MAKTABA

Mwanasiasa mkongwe Charles Mugane yu hai na buheri wa afya tofauti na madai yaliyoenezwa hapo awali kwamba ameaga dunia.

Familia ya mwanasheria huyo mkuu wa kwanza nchini imepuuzilia mbali uvumi kuhusu kufariki kwake na kudai kuwa ni ripoti zilizotiwa chumvi.

Ujumbe ambao ulitolewa na familia yake kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili umethibitisha kwa Njonjo ako salama salimini na anafurahia wikendi akiwa nyumbani kwake.

"Ripoti kuhusu kifo changu zimetiwa chumvi. Niko buheri wa afya na nafurahia wikendi yangu nyumbani tunaposherehekea siku ya Utamaduni" Ujumbe huo ulisoma.

Uvumi kuhusu kifo cha mkongwe huyo wa miaka 101 ulienezwa sana mitandaoni siku ya Jumamosi.

Wengi walijipata wakiamini madai hayo kutokana na kiwango kiubwa cha ripoti kuhusu kifo chake ambazo zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii.