Mwanamke aliyetilia maafisa wa kaunti ya Kisumu 'mchele' kwa pombe ainywa mwenyewe bila kujua na kuzirai

Muhtasari

•Maafisa wa DCI wamesema kuwa Leah alipoteza fahamu baada ya kunywa pombe ambayo alikuwa ametia dawa bila kujua alikuwa ameweka mtego wa kujitega mwenyewe.

crime scene 1
crime scene 1

Polisi katika kaunti ya Mombasa wanazuilia mwanamke mmoja anayeaminika kuwa mmoja wa genge la wanawake wanaotilia watu dawa za kuwafanya wapoteze fahamu kwa vinyweo wakiwa na nia ya kuwaibia.

Leah Mwenja ,31, alikamatwa siku ya Jumamosi baada ya kupatikana akiwa amepoteza fahamu pamoja na wanaume watatu katika jengo la Shirika eneo la Nyali, Mombasa.

Maafisa wa DCI wamesema kuwa Leah alipoteza fahamu baada ya kunywa pombe ambayo alikuwa ametia dawa bila kujua alikuwa ameweka mtego wa kujitega mwenyewe.

Inaripotiwa kuwa Leah pamoja na wanawake wengine wawili walikuwa wametega maafisa wawili wa kaunti ya Kisumu na MCA mmoja kwa urembo na mavazi yao mafupi hadi wakaalikwa kujiburudisha nao.

Sita hao walijiburudisha na kunywa vileo vingi hadi mida ya saa tisa usiku ambapo wanawake wale walishawishi maafisa hao wa kaunti waelekee kwa chumba chao ili wafanye yale ambayo hawangefanya hadharani.

Bila kufahamu hatari iliyokuwa mbele yao, maafisa hao wa kaunti waliandamana na wanadada wale watatu hadi kwa chumba chao wakiwa wamebeba chupa zaidi za pombe ambazo walikusudia kunywa wakiwa wanajiburudisha kwa nyumba.

Maafisa wengine wa kaunti ambao walikuwa wameandamana na wahasiriwa kwa ziara ya kazi ndio waliowapata wakiwa wamepoteza fahamu ndani ya chumba chao asubuhi ya Jumamosi.

Kando yao alilala mshukiwa ambaye alikuwa kajiroga mwenyewe bila kujua.

Wenzake Leah hata hivyo walikuwa washatoroka baada ya kugundua kuwa mwenzao alikuwa amepoteza fahamu. Waliiba vipakatalishi, simu na bidhaa zingine za maafisa hao.

Wahasiriwa walipokea matibabu katika hospitali ya Coast General huku wapelelezi kutoka kituo cha Nyali wakimzuia Leah na kumhoji ili awapatie taarifa kuhusu walikojificha wenzake.