Rais Kenyatta atupilia mbali uamuzi wa ICJ katika kesi ya mpaka kati ya Kenya na Somalia, aapa kulinda eneo linalozozaniwa

Muhtasari

•Rais amepuuzilia mbali uamuzi wa mahakama ya ICJ wa kupatia Somalia kipande kikubwa cha bahari ya Hindi ambacho kilikuwa kinazozaniwa huku akiapa kuwa Kenya haitatambua uamuzi huo.

•Kenyatta amesema kuwa uamuzi wa ICJ waweza kuathiri uhusiano wa Kenya na Somalia huku akitoa pendekezo kwa jumuiya ya kimataifa kuunda mazingira ambayo yatawezesha maafikiano kupatikana kwa njia ya mazungumzo

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta hatimaye  amezungumza baada ya mahakama ya kimataifa (ICJ) kutoa uamuzi wa kesi ya mpaka wa bahari kati  ya Kenya na Somalia.

Rais amepuuzilia mbali uamuzi wa mahakama ya ICJ wa kupatia Somalia kipande kikubwa cha bahari ya Hindi ambacho kilikuwa kinazozaniwa huku akiapa kuwa Kenya haitatambua uamuzi huo.

"Kenya haijashangazwa na uamuzi huo, kuna wasiwasi  kuhusiana na kuagizwa kwa uamuzi na maana yake kwa eneo la pembe ya Afrika na sheria ya kitaifa kwa jumla. Kenya ingependa kusema kuwa inatupilia mbali na haitatambua uamuzi huo" Rai s alisema kupitia ujumbe wa kuchapishwa.

Rais alisema kuwa  hapo awali Kenya ilikuwa imekubali kushiriki kwenye kesi hiyo licha ya kuwa mahakama ya ICJ  na mamlaka na uwezo wa kusuluhisha mzozo uliokuwepo.

Amesema kuwa Kenya ililazimika kuijiondoa kwenye kesi hiyo mnamo Machi  14  kufuatia malalamishi ya upendeleo  wa majaji ulioegemea upande wa Somalia.

Kenyatta amesema kuwa uamuzi wa ICJ waweza kuathiri uhusiano wa Kenya na Somalia huku akitoa pendekezo kwa jumuiya ya kimataifa kuunda mazingira ambayo yatawezesha maafikiano kupatikana kwa njia ya mazungumzo

"Kenya na Somalia ni majirani ambao wana mpaka mmoja na wana tamaduni za pamoja. Uamuzi huo utazorotesha uhusiano kati ya mataifa mawili husika. Pia utazorotesha mafanikio ya kijamii, siasa na uchumi na kuna uwezekano  wa kuzidisha hofu ya usalama katika eneo la pembe ya Afrika" Kenyatta alisema.

Rais ameapa kulinda eneo la nchi linalozozaniwa kwa njia zote kama alivyoahidi wakati alikuwa anakula kiapo cha ofisi

"Nilikula kiapo kulinda mipaka ya taifa la Kenya. Sina nia ya kukaidi kiapo changu na nitafanya kila kitu kama rais na kamanda mkuu wa jeshi kuhifadhi eneo la nchi hii na nipishe hayo kwa rais atakayechukua zamu baada ya muhula wangu kuisha mwaka ujao" Rais aliapa.

Hata hivyo rais amesema kuwa Kenya itatumia taasisi kama Umoja wa Afrika (UN) na njia zingine za majadiliano ya pande zote mbili kusuluhisha mzozo.