Mume wa mwanariadha aliyeuawa Agnes Tirop akamatwa huko Mombasa

Muhtasari
  • Mume wa mwanariadha aliyeuawa Agnes Tirop akamatwa huko Mombasa
Agnes Tirop
Image: Hisani

Mume wa Mshikilizi wa rekodi ya ulimwengu Agnes Tirop amekamatwa huko Changamwe, Mombasa juu ya mauaji yake huko Iten.

Kulingana na taarifa ya polisi, mtuhumiwa alikuwa akiendesha gari la kibinafsi wakati alipokamatwa.

Tirop, 25, alikuwa sehemu ya timu ya ushindi iliyowakilisha Kenya katika Olimpiki za Tokyo za 2020; ambapo aliwakilisha nchi katika mbio za mita 5,000 na kumaliza wa nne katika fainali.

Bingwa huyo wa Kenya alipatikana amekufa nyumbani kwake huko Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet Jumatano.

Siku ya Jumatano, wachunguzi wa eneo la uhalifu walikuwa nyumbani kwa Tirop, ambaye polisi wanasema aliripotiwa kupotea na baba yake Jumanne usiku.

"[Polisi] walipoingia nyumbani, walimkuta Tirop kwenye kitanda na kulikuwa na damu sakafuni," Tom Makori, mkuu wa polisi wa eneo hilo, alisema.