Mwanamke aliyeficha jamaa mvunguni mwa kitanda ili asiuawe na majambazi apigwa risasi Meru

Muhtasari

•Kulingana na DCI, washukiwa hao walimpiga mhasiriwa risasi alipokataa kufichua alikokuwa amejificha mwendesha bodaboda ambaye walikuwa wanataka kuangamiza.

•Kufuatia hayo Mutwiri alitoka mvunguni mwa kitanda  na kusaidiana na majirani waliofika kwenye eneo la tukio kumpeleka mhasiriwa hospitalini ambako anaendelea kupokea matibabu

Picha ya Bunduki
Picha ya Bunduki
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ya Meru wanawasaka washukiwa wawili wanaodaiwa kumpiga risasi mwanamke mmoja aliyeficha jamaa ambaye walikuwa wanakimbiza.

Kulingana na DCI, washukiwa hao walimpiga mhasiriwa risasi alipokataa kufichua alikokuwa amejificha mwendesha bodaboda ambaye walikuwa wanataka kuangamiza.

Inaripotiwa kuwa mwendesha bodaboda aliyetambulishwa kama Eliphas Mutwiri alikuwa amebeba washukiwa hao wawili  kutoka soko ya Laare eneo la Igembe kuwapeleka katika soko ya Joune wakati mmoja wao alitoa bastola na kumuagiza asimamishe pikipiki.

Mutwiri alisita kusimama kama alivyokuwa ameagizwa na kujaribu kumnyang'anya mhalifu yule bastola. Katika harakati ile risasi moja ilifyatuka kutoka kwa bastola na hapo pikipiki ikaanguka na Mutwiri akatoroka upesiupesi.

Wakati washukiwa wale walikuwa wanang'ang'ana kuamka baada ya kulaliwa na pikipiki Mutwiri alikimbia kwa nyumba jirani ambapo alikaribishwa na mwanamke aliyemwelekeza ajifiche chini ya kitanda.

Dakika chache baadae,wahalifu wale walivamia nyumba hiyo na kuamuru mwanamke yule awaambie alikokuwa amejificha Mutwiri, Mwanamke yule alisita kutoa taarifa zozote na hapo mshukiwa aliyekuwa amebeba bastola akampiga risasi kwenye mguu wake wa kushoto kisha wakatoroka wote wawili.

Kufuatia hayo Mutwiri alitoka mvunguni mwa kitanda  na kusaidiana na majirani waliofika kwenye eneo la tukio kumpeleka mhasiriwa hospitalini ambako anaendelea kupokea matibabu