Mbunge wa Kisumu ya kati akamatwa kuhusiana na ghasia

Muhtasari

• Kamanda wa polisi wa kaunti ya Kisumu Kipkirui Ng’eno alithibitisha kuwa wanamzuilia mbunge kama mahabusu.

• Mmoja wa wathiriwa alipata majeraha mabaya kichwani, mbavu, jicho na kidevu wakati wa patashika hizo.

Uharibifu katika mkahawa Kolongolo
Uharibifu katika mkahawa Kolongolo
Image: MAURICE ALAL

Mbunge wa Kisumu ya Kati Fred Ouda amekamatwa kwa madai ya uvamizi na vurugu za kisiasa katika hoteli moja mjini Kisumu siku ya Ijumaa.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Kisumu Kipkirui Ng’eno alithibitisha kuwa wanamzuilia mbunge kama mahabusu.

Watu watatu walijeruhiwa wakati mbunge huyo alipodaiwa kuvamia hoteli hiyo akiandamana na baadhi ya wafuasi wake na kuwashambulia wale alioonekana kuwa wafuasi wa mfanyabiashara ambaye pia anawania kiti cha Kisumu ya kati Joshua Oron.

Bidhaa za thamani isiyojulikana ziliharibiwa wakati wa tukio la Ijumaa katika mkahawa wa Kalongolongo katika mtaa wa Milimani.

Mmoja wa waliojeruhiwa wakati wa makabiliano katika mkahawa wa Kolongolo
Mmoja wa waliojeruhiwa wakati wa makabiliano katika mkahawa wa Kolongolo
Image: MAURICE ALAL

Kamanda wa polisi alisema Ouda anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kisumu Central.

"Tuna mbunge huyo kwenye seli ya polisi na bado tunachunguza tukio hilo," Ngeno alisema.

Ngeno alisema Ouda anashikiliwa kwa madhumuni ya kuhojiwa. "Tunamshikilia kwa madai ya uchochezi na uharibifu wa mali," alisema.

Oron alikuwa kwenye mkahawa wakati wa tukio hilo.

Oron anataka kutwaa kiti cha Ouda ambaye anatumikia muhula wake wa kwanza.

Mmoja wa wathiriwa alipata majeraha mabaya kichwani, mbavu, jicho na kidevu wakati wa patashika hizo.

Alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kisumu kwa matibabu. "Nimepelekwa xray. Nitaripoti shambulio hilo kwa polisi kwa hatua zinazofaa," aliiambia Star.

Waathiriwa wengine wawili akiwemo mwanamke pia walikimbizwa katika hospitali ya Kisumu.

IMETAFSIRIWA NA KUHARIRIWA NA DAVIS OJIAMBO