Seneta wa Lamu Anuar aachiliwa kwa dhamana

Muhtasari

• Anuar anatuhumiwa kwa kumpiga risasi na kumjeruhi mwanamke  katika kisa kilichotokea kwenye hoteli moja mjini Nanyuki.

• Mhasiriwa alidai kwamba ugomvi ulizuka baina yake na seneta kabla yake kuchukua bunduki na kumpiga risasi kwa karibu.

Image: HISANI

Seneta wa Lamu Anuar Loitiptip ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi nusu milioni pesa taslim au shilingi milioni moja na hakikisho lenye thamani sawa baada ya kushtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya bunduki.

Seneta huyo pia ameagizwa kuripoti kwa ofisi za DCI kila baada ya siku mbili.

Anuar anatuhumiwa kwa kumpiga risasi na kumjeruhi mwanamke  katika kisa kilichotokea kwenye hoteli moja mjini Nanyuki.

Alijisalimisha kwa polisi siku ya Jumapili baada ya taarifa kuenea kuwa anatafuta kufuatia madai kwamba alipimga risasi mwanamke mjini Nanyuki.

Seneta huyo alikesha katika kituo cha polisi cha Nanyuki akisubiri kufikishwa mahakamani.

Bunduki yake ilichukuliwa punde tu baada ya kujisalimisha na itafanyiwa ukaguzi kama sehemu ya uchunguzi.

Anwar anaripotiwa kuambia polisi kwamba alishambuliwa akiwa katika eneo la burudani, jambo ambalo llilifanya afyatue risasi na kumjeruhi Joy Makena (32).

Bi Makena alikimbizwa katika hospitali ya Nanyuki akiwa na jeraha ya risasi kwenye mguu wake wa kulia. Aliambia polisi kwamba alipigwa risasi na seneta Anuar.

Mhasiriwa alidai kwamba ugomvi ulizuka baina yake na seneta kabla yake kuchukua bunduki na kumpiga risasi kwa karibu.