Utovu shuleni: moto wateketeza shule tano je kunani?

Muhtasari

•Shule hizo ni pamoja na Mwala Girls High katika Kaunti ya Machakos, Maranda High katika Kaunti ya Siaya, Cheplaskei High iliyoko Uasin Gishu, Shule ya Upili ya Wavulana ya Nambale iliyoko Busia na Shule ya Msingi ya St. Mary's Riabore katika Kaunti ya Nyamira.

•Haya yanajiri huku polisi wakisema wako tayari kuwafungulia mashtaka wanafunzi wawili kutoka shule ya upili ya wasichana ya Buruburu kutokana na kisa cha moto kilichotokea katika shule hiyo wiki jana na kupelekea kujeruhiwa kwa wanafunzi 59.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Shule tano zaidi zimeripoti visa vya moto katika muda wa saa 14 zilizopita nchini.

Shule hizo ni pamoja na Mwala Girls High katika Kaunti ya Machakos, Maranda High katika Kaunti ya Siaya, Cheplaskei High iliyoko Uasin Gishu, Shule ya Upili ya Wavulana ya Nambale iliyoko Busia na Shule ya Msingi ya St. Mary's Riabore katika Kaunti ya Nyamira.

Mamlaka ya polisi inasema wanatarajia matukio hayo kuendelea kuongezeka kutokana na uchochezi.

Haya yanajiri huku polisi wakisema wako tayari kuwafungulia mashtaka wanafunzi wawili kutoka shule ya upili ya wasichana ya Buruburu kutokana na kisa cha moto kilichotokea katika shule hiyo wiki jana na kupelekea kujeruhiwa kwa wanafunzi 59.

Wawili hao wanadaiwa kupanga na kuchoma moja ya vyumba katika bweni moja mnamo Oktoba 31 kabla ya kutoroka na kuwaacha wenzao nyuma.

Inadaiwa walisikika wakipanga kuchoma moja ya vyumba na baadaye kuonekana wakiondoka kutoka eneo la tukio huku moto ukizuka.

Takriban wanafunzi wengine 16 kutoka shule ya upili ya Kakamega wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kutokana na tukio la moto katika shule hiyo.

Wanafunzi wa kidato cha nne na tatu katiks shule ya Buruburu Girls wanatarajiwa kurejea shuleni leo (Jumatatu) huku wenzao wa kidato cha kwanza na cha pili wakitarajiwa kurejea kesho Jumanne.

Bodi ya usimamizi na muungano wa wazazi na walimu walishiriki kikao Alhamisi iliyopita na maazimio kadhaa ambayo ni pamoja na uwekaji wa kamera za CCTV shuleni hapo, kuwepo kwa milango Iliyofunguliwa kwenda nje moja kwa moja na kukuguliwa mara kwa mara, mataa kuwekwa ili kufanikisha usalama na kuondolewa kwa milango yote ya vyumba vilivyo kwa bweni ili kurahisisha harakati katika kesi ya dharura.

Baadhi ya wazazi shuleni hapo wamelalamikia uamuzi uliofikiwa na uongozi wa shule kuwataka wanafunzi wote kulipa shilingi 1,500 kwa uharibifu uliotokea wakati wa moto huo.

Wanasema kuwa hasara iliyopatikana haipaswi kugharamiwa na wazazi wote.

Mzigo wa kujenga upya shule umesukumiwa wazazi baada ya serikali kutangaza wiki jana kwamba haitasaidia katika kujenga upya mabweni yaliyoharibiwa na moto wa shule.

(Utafsiri: Samuel Maina)