Wafanyibiashara watatu wakamatwa na Heroin yenye thamani ya Sh3M Kilifi

Muhtasari

•Swalehe Yusuf Ahmed na Suleiman Salim Kaingu walikamatwa katika eneo la Kikambala, kaunti ya Kilifi wakiwa na vifurushi kadhaa vya takriban kilo moja ya Heroin inayokadiriwa kuwa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu katika soko haramu

•Hapo awali Swalehe alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa zaidi ya kilo 105 za Heroin ambayo ilikadiriwa kuwa yenye thamani ya shilingi milioni 285.  Mshukiwa aliachiliwa kwa dhamana baada ya kukanusha mashtaka.

Image: TWITTER// DCI

Polisi katika kaunti ya Mombasa wanazuilia washukiwa watatu wa ulanguzi wa madawa ya kulevya ambao walikamatwa siku ya Jumanne na wapelelezi wa uhalifu uliopangwa kimataifa.

Kulingana na taarifa ambayo ilitolewa na DCI siku ya Jumatano, watatu hao wamekuwa wakiendeleza biashara hiyo haramu hapa nchini na nje ya mipaka bila kupatikana wala kuadhibiwa.

Swalehe Yusuf Ahmed na Suleiman Salim Kaingu walikamatwa katika eneo la Kikambala, kaunti ya Kilifi wakiwa na vifurushi kadhaa vya takriban kilo moja ya Heroin inayokadiriwa kuwa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu katika soko haramu.

Susan Mukonyo Mutuku ambaye ni mhudumu wa duka la Mpesa pia alikamatwa pamoja na washukiwa hao wawili kwani anaaminika kutumiwa na mshukiwa mkuu kutakatisha mapato yake ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Inaripotiwa kuwa Swalehe anajulikana kama muuzaji sugu wa madawa katika eneo la Pwani na tayari ana kesi zingine mbili kortini zinazohusiana na biashara ile haramu.

Hapo awali Swalehe alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa zaidi ya kilo 105 za Heroin ambayo ilikadiriwa kuwa yenye thamani ya shilingi milioni 285.  Mshukiwa aliachiliwa kwa dhamana baada ya kukanusha mashtaka.

Swalehe, Suleiman na Susan walifikishwa katika mahakama ya Mombasa siku ya Jumatano kwa maombi mbalimbali ili kuwezesha uchunguzi kukamilika siku ya Alhamisi.