Ibrahim Rotich akana kuua aliyekuwa mpenzi wake, mwanariadha Agnes Tirop

Rotich alipatikana kuwa mzima na tayari kujibu mashtaka

Muhtasari

•Rotich alifikishwa mbele ya jaji Reuben Nyakundi wa mahakama kuu ya Eldoret na kukanusha mashtaka ya mauaji ambayo alisomewa

•Kupitia kwa wakili wake Ngige Ngugi Rotich amedokeza kuwa ataomba kuachiliwa kwa bondi kesi zikiendelea.

Ibrahim Rotic katika mahakama kuu ya Eldoret mnamo Novemba 16, 2021
Ibrahim Rotic katika mahakama kuu ya Eldoret mnamo Novemba 16, 2021
Image: MATHEWS NDANYI

Habari na Mathews Ndanyi

Ibrahim Kipkemboi Rotich amekanusha mashtaka ya kuua aliyekuwa mpenzi wake Agnes Tirop mnamo Oktoba 12.

Rotich alifikishwa mbele ya jaji Reuben Nyakundi wa mahakama kuu ya Eldoret na kukanusha mashtaka ya mauaji ambayo alisomewa.

Kupitia kwa wakili wake Ngige Ngugi Rotich amedokeza kuwa ataomba kuachiliwa kwa bondi kesi zikiendelea.

Hata hivyo wakili wa serikali David Fedha amesema tayari wamewasilisha kesi ya kupinga maombi hayo ya bondi.

Jaji Nyakundi ameagiza kesi hiyo itajwe tena mnamo Desemba 1 kwa maelekezo zaidi.

Wiki iliyopita mahakama iliamuru mshukiwa ambaye alikuwa mume wa marehemu apelekwe katika hospitali ya rufaa ya Moi kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kushtakiwa.

Wakili wa serikali David Fedha alisema ni sharti mshukiwa angefanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kusomewa mashtaka ya kuua mwanariadha Tirop.

Rotich alipatikana kuwa mzima na tayari kujibu mashtaka.

Mwili wa Tirop ulipatikana ndani ya nyumba yake katika eneo la Iten mnamo Oktoba 13 mwakani.

Uchunguzi wa maiti ulibaini kuwa marehemu aliaga baada ya kudungwa kwenye shingo na kugongwa kichwani na silaha butu.