Miguna Miguna akwama katika uwanja wa ndege Ujerumani baada ya kuzuiwa kurejea Kenya

Muhtasari

•Miguna alifahamisha Wakenya kuwa alipatiwa taarifa kuhusu hali hiyo alipokuwa katika kituo cha ndege cha Berlin Brandenburg  nchini Ujerumani tayari kuabiri ndege ya kurejea hapa nchini.

•Miguna alikuwa amekata tikiti ya ndege ya kusafiri kutoka Kanada kupitia Ujerumani na Ufaransa kutua Kenya leo, Novemba 16.

•Siku ya Ijumaa jaji Hedwig Ong'undi alisema hakuna ushahidi kuwa Miguna amezuiwa kurejea nchini.

Image: TWITTER// MIGUNA MIGUNA

Kuna uwezekano mkubwa sana wakili na mwanasiasa mashuhuri Miguna Miguna atakosa  kuwasili nchini siku ya Jumanne kama ilivyotarajiwa baada ya kampuni ya usafiri ya wa ndege 'Air France'  kumuonyesha barua ya tahadhari 'Red alert' kutoka Kenya jioni ya Jumatatu.

Hii inamaanisha kwamba makampuni ya ndege hayana uwezo wa kumsafirisha hadi Kenya.

Kupitia ujumbe ambao alichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumatatu jioni, Miguna alifahamisha Wakenya kuwa alipatiwa taarifa kuhusu hali hiyo alipokuwa katika kituo cha ndege cha Berlin Brandenburg  nchini Ujerumani tayari kuabiri ndege ya kurejea hapa nchini.

"Hii ni kuwafahamisha Wakenya na ulimwengu mzima kwamba maafisa wa AirFrance katika kaunta ya kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Berlin Brandenburg wamenifahamisha punde tu kwamba Serikali ya Kenya iliwatumia "Red Alert" asubuhi ya leo kwamba hawawezi kunisafirisha hadi Nairobi. Bado nasubiri nakala" Miguna aliandika.

Mshauri huyo wa siasa wa zamani wa kinara wa ODM Raila Odinga aliambatanisha ujumbe wake na barua ambayo alidai kupokea kutoka kwa kampuni ya Air France.

Kulingana na barua hiyo, Miguna alikuwa amekata tikiti ya ndege ya kusafiri kutoka Kanada kupitia Ujerumani na Ufaransa kutua Kenya leo, Novemba 16.

"Wamekataa kutaja "Red Alert." Lakini wameonyesha kuwa ni dhahiri wananihurumia lakini hakuna wanachoweza kufanya. Wacha mawakili waanze kazi sasa. Asante kwa wote. Aluta Continua" Alisema Miguna.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mahakama kuu kukataa kutupilia mbali vikwazo ambavyo serikali ya Kenya imewekea Miguna kurejea nchini.

Siku ya Ijumaa jaji Hedwig Ong'undi alisema hakuna ushahidi kuwa Miguna amezuiwa kurejea nchini.

Miguna, ambaye ana uraia wa Kenya na Kanada, alifurushwa kutoka Kenya mnamo Februari 2018 baada ya kushiriki katika kuapishwa kwa Raila kama 'Rais wa Watu' katika uwanja wa Uhuru Park mnamo Januari 30, 2018.