Mahabusu wawili waliokuwa wametoroka korokoroni wakamatwa tena Kisumu

Muhtasari

•Mohammed Aden Hussein (18) na Elvis Odhiambo (17)  walikamatwa mwendo wa saa mbili asubuhi ya Jumatano na timu ya maafisa kutoka kituo cha Kondele na Kapsoya.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Kisumu wamewakamata tena washukiwa wawili wa wizi wa mabavu ambao walikuwa wametoroka kutoka korokoroni wiki iliyopita.

Mohammed Aden Hussein (18) na Elvis Odhiambo (17)  walikamatwa mwendo wa saa mbili asubuhi ya Jumatano na timu ya maafisa kutoka kituo cha Kondele na Kapsoya.

Wawili hao walikuwa wametoroka kutoka kituo cha polisi cha Kapsoya tarehe mnamo Novemba 11  ambapo walikuwa wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa katika mahakama ya Eldoret kujibu mashtaka ya wizi wa mabavu.

Baada ya kukamatwa kena washukiwa walizuiliwa katika kituo cha Kondele wakisubiri kurejeshwa katika kituo cha Kapsoya.

Haya yanajiri huku visa vya wafungwa kutoroka magerezani vikiwa vimekithiri hapa nchini.

Asubuhi ya Jumatatu washukiwa wafungwa watatu wa ugaidi walitoroka katika gereza ya Kamiti.

Polisi walisema Musharaf Abdalla Akhulunga almaarufu Zarkawi/Alex/Shukri, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo almaarufu Yusuf walitoroka katika kituo cha kurekebishia tabia chenye ulinzi mkali mwendo wa saa moja asubuhi.

Zawadi ya shilingi milioni 60 ilitolewa kwa yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kukamatwa kwa wafungwa hao ambao walisemekana kuwa hatari sana.

Walinzi saba katika gereza hiyo walikamatwa kufuatia kutoroka kwa wafungwa hao.