DCI Kinoti ahukumiwa kifungo cha miezi minne gerezani

Muhtasari

•Amehukumiwa kifungo cha miezi minne kwa kukaidi amri ya mahakama iliyomtaka aachilie bunduki zinazomilikiwa na mfanyibiashara Jimi Wanjigi

•Mahakama imeamuru Kinoti ajisalimishe gerezani ndani ya kipindi cha siku saba zijazo huku  Inspekta Jenerali wa polisi  akiagizwa atoe amri ya kakamatwa kwake iwapo atakaidi amri hiyo.

DCI George Kinoti
DCI George Kinoti
Image: MAKTABA

DCI George Kinoti amehukumiwa kifungo cha miezi minne kwa kukaidi amri ya mahakama iliyomtaka aachilie bunduki zinazomilikiwa na mfanyibiashara Jimi Wanjigi.

Mahakama imeamuru Kinoti ajisalimishe gerezani ndani ya kipindi cha siku saba zijazo huku  Inspekta Jenerali wa polisi  akiagizwa atoe amri ya kakamatwa kwake iwapo atakaidi amri hiyo.

Mnamo Januari 2019 hakimu  Anthony Mrima alikuwa ameagiza DCi, Inspekta Jenerali wa polisi na DPP warejeshe bunduki zote na silaha ambazo zilichukuliwa katika makao ya Wanjigi mwaka wa 2017.

Silaha zinazodaiwa ni pamoja na bastola moja, Smith & Wesson moja , bastola aina ya Glock, bunduki moja ya kivita kati ya zingine.

Alipokuwa anatoa agizo hilo, jaji Mrima alisema serikali ilitenda bila mantiki kuchukua bunduki za Wanjigi ilhali bado ana leseni halali.

Wanjigi amewasilisha kesi ya kukaidi amri ya mahakama dhidi ya DCI kwa kukosa kutii maagizo ya jaji na kuomba wafungwe katika jela ya kiraia.

DCI anasema wamekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mrima na suala hilo bado linashughulikiwa  katika mahakama ya kukata rufaa.

Kinoti DCI anadai kuwa baadhi ya bunduki zinazomilikiwa na Wanjigi ni za kijeshi na zenye usahihi wa hali ya juu ambazo hazijaidhinishwa kumilikiwa na raia nchini Kenya chini ya Sheria ya Silaha za Moto.