Mahakama yazuia shule ya Kakamega kuwaadhibu wanafunzi kufuatia moto ulioteketeza bweni

Muhtasari

•Mzazi mmoja, Boaz Vida alikuwa amewasilisha kesi mahakamani akiomba shule hiyo isitoze kila mwanafunzi shilingi 9, 823 kugharamia uharibifu uliosababishwa na moto.

•Mzazi huyo analalamika kuwa maamuzi hayo yalipitishwa bila kuwashirikisha wazazi, kitendo ambacho ni cha adhabu na ni kinyume cha katiba.

•Vida analalamika kuwa haikuwa haki kuwaadhibu wanafunzi 20 waliokuwa darasani wakati wa moto huo kwa kubeba jukumu la juu zaidi.

Lango la shule ya upili ya Kakamega
Lango la shule ya upili ya Kakamega
Image: HILTON OTIENO

Mahakama kuu ya Kakamega imezuia kutekelezwa kwa uamuzi wa usimamizi wa shule ya upili ya Kakamega kuwatoza wazazi kwa uharibifu uliosababishwa na moto ulioteketeza mabweni mawili ya shule hiyo mnamo Novemba 5.

Mzazi mmoja, Boaz Vida alikuwa amewasilisha kesi mahakamani akiomba shule hiyo isitoze kila mwanafunzi shilingi 9, 823 za kugharamia uharibifu uliosababishwa na moto.

Vida amemtaja mwalimu mkuu wa shule hiyo, Gerald Oruna ambaye ni katibu wa bodi ya wasimamizi wa shule pamoja na mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Egara Kabaji, kama wajibu mashtaka wa kwanza na wa pili mtawalia.

Bodi ya usimamizi wa shule hiyo ilikutana mnamo Novemba 10 na kukubaliana kila mwanafunzi alipe shilingi 9, 823 kugharamia uharibifu uliotokea na tarehe wanafunzi wakatengewa tarehe za kurudi shule kuanzia na wale wa kidato cha nne ambao walirudi siku ya Jumatatu.

Wanafunzi wa kidato cha kwanza wanatarajiwa kurudi siku ya Jumapili, wa kidato cha  pili warudi Jumanne na wale wa kidato cha tatu warudi Alhamisi.

 

Shule hiyo ilitathmini uharibifu kuwa shilingi 12,185,540. Wazazi walitozwa shilingi 695,420 zaidi za kuweka camera za CCTV, shilingi 4,194,400 zakununua vitanda 280  vya ghorofa ambavyo viliteketea pamoja na vitu vya wanafunzi vya thamani ya  shilingi milioni 4.5 ambavyo viliharibiwa.

Jaji William Musyoka aliagiza mlalamishi awakabidhi walalamikiwa malalamishi yake ifikapo siku ya Jumanne wiki ijayo na kuelekeza kesi hiyo ing'oe nanga mnamo Novemba 30.

Mzazi huyo analalamika kuwa maamuzi hayo yalipitishwa bila kuwashirikisha wazazi, kitendo ambacho ni cha adhabu na ni kinyume cha katiba.

Uamuzi huo pia ni kinyume cha sheria kwa vile unakiuka kanuni ya 36 (3) ya Kanuni za Elimu ya Msingi za mwaka 2015.

Vida analalamika kuwa haikuwa haki kuwaadhibu wanafunzi 20 waliokuwa darasani wakati wa moto huo kwa kubeba jukumu la juu zaidi.

(Utafsiri: Samuel Maina)