Mahabusu watatu watoroka kutoka kizuizini Narok

Muhtasari

•Shadrack Leparan  ,Enocj Ndege  na Patrick Mausa  wanaripotiwa kutoroka usiku wa kuamkia Jumamosi  baada ya kufanikiwa kutoboa shimo kwenye ukuta wa seli ambayo walikuwa wamewekwa

•Kufuatia hayo polisi watatu ambao walikuwa katika zamu usiku wa kuamkia Jumamosi wametiwa mbaroni.

Jail bars
Jail bars
Image: FREEPIK

Huku visa vya wafungwa na mahabusu kutoroka vikiwa vimekithiri nchini washukiwa wengine watatu wanaripotiwa kutoroka kutoka kituo cha polisi cha Kilgoris, kaunti ya Narok ambako walikuwa wanazuiliwa.

Shadrack Leparan  ,Enocj Ndege  na Patrick Mausa  wanaripotiwa kutoroka usiku wa kuamkia Jumamosi  baada ya kufanikiwa kutoboa shimo kwenye ukuta wa seli ambayo walikuwa wamewekwa. Watatu hao walikuwa wafikishwe mahakamani Jumatatu.

Kufuatia hayo polisi watatu ambao walikuwa katika zamu usiku wa kuamkia Jumamosi wametiwa mbaroni.

Maafisa hao, Carmax Okelo, Andrew  Bett na Jalus Okoa watahojiwa kueleza jinsi mahabusu watatu walifanikiwa kutoroka wakati walikuwa wameshika doria.

Haya yanajiri siku mbili tu baada ya washukiwa wa kigaidi ambao walitoroka katika jela ya Kamiti siku ya Jumapili kukamatwa katika eneo la Mwingi, kaunti ya Kitui.

Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi walikamatwa alasiri ya Alhamisi wakiwa safarini kuelekea nchi jirani ya Somalia.

Serikali ilikuwa imetoa ahadi ya shilingi milioni 60 kwa yeyote ambaye angetoa habari ambazo zingesaidia kukamatwa kwa washukiwa hao.