Wanaume katika kaunti ya Meru walalamika kuhusu baridi vitandani

Muhtasari

• Baadhi ya wanaume wana wasiwasi kwamba ndoa zao zinaelekea kuvunjika kutokana na utoro wa wake zao wanaokwenda kuchota maji kwenye mkondo mdogo, jambo ambalo huchukua muda mwingi.

Wanawake wakichota maji
Wanawake wakichota maji
Image: MAKTABA

Wanaume kutoka kijiji cha Karama, kata ya Akirangondu, eneo bunge la Igembe ya Kati wametaharuki kutokana na uhaba wa maji unaowafanya wake zao wasilale kitandani usiku kucha.

Wanalalamika kuwa uhaba wa maji umewalazimu wake zao kukesha mchana na usiku nje ya nyumba zao badala ya kupasha joto vitanda vyao.

 Baadhi ya wanaume wana wasiwasi kwamba ndoa zao zinaelekea kuvunjika kutokana na utoro wa wake zao wanaokwenda kuchota maji kwenye mkondo mdogo, jambo ambalo huchukua muda mwingi.

"Tuna njaa kwenye vitanda vya baridi huku wake zetu wakitumia saa nyingi haswa usiku wakingoja foleni ndefu za mitungi na kutufanya tukose haki zetu za ndoa," analalamika mkazi, Ntarangwi Karithi.

 Wakazi hao waliiomba serikali ya kaunti kuchimba kisima ili kupunguza msongamano kwenye mkondo huo mdogo na kuepuka kutoroka kwa wake zao mchana na usiku.

 Walimkashifu MCA wa eneo hilo Richard Gitari kwa kuzembea na kuwatenga wakati wa ugawaji wa miradi, huku wakiitaka zaidi serikali ya kaunti kupitia gavana huyo kuingilia kati.

 Aidha walibaini kuwa mbali na ndoa zao kuwa hatarini, watoto na wake zao wako kwenye hatari ya kukosa usalama nyakati za usiku.

Pia walieleza kuwa mkondo huo mdogo unakuwa na matope na kuwaweka katika hatari ya magonjwa yatokanayo na maji.

Juhudi za kufikia MCA wa eneo hilo kwa njia ya simu hazikuzaa matunda.

(Utafsiri: Samuel Maina)