Afisa wa polisi auawa Marakwet

Muhtasari

• Afisa huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Chebiemit na baadaye kuhamishiwa hadi hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi (MTRH) mjini Eldoret.

• Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Marakwet Magharibi John Matasi alisema afisa huyo alithibitishwa kufariki alipofika katika hospitali ya rufaa.

• Mshukiwa kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi akisubiri kufikishwa mahakamani huku mwili wa afisa wa polisi ukihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha MTRH ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

crime scene
crime scene

Afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Kaptabuk eneo la Koibarak Kaunti Ndogo ya Marakwet Magharibi ameuawa na mwanakijiji.

Afisa huyo, Julius Mengich Kipserem, pamoja na mwenzake Morrison Ndungu, walikuwa wakijibu malalamishi yaliyowasilishwa na Wesley Biwott Chemisto jana saa tisa jioni kuhusu mtu aliyejulikana tu kama Adam ambaye alidaiwa kuiba mahindi kutoka kwa shamba lake.

Walipofika eneo la tukio, walivamiwa na nduguye mshukiwa Eliud Kipgosgei na katika purukushani hiyo, alimchoma Kipserem kichwani kwa mshale unaoshukiwa kuwa na sumu.

Afisa huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Chebiemit na baadaye kuhamishiwa hadi hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi (MTRH) mjini Eldoret.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Marakwet Magharibi John Matasi alisema afisa huyo alithibitishwa kufariki alipofika katika hospitali ya rufaa.

Mhusika kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi akisubiri kufikishwa mahakamani huku mwili wa afisa wa polisi ukihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha MTRH ukisubiri kufanyiwa upasuaji.