Mshtuko baada ya chifu kupatikana akiwa amejitia kitanzi ndani ya ofisi Murang'a

Muhtasari

•Inadaiwa Macharia alijitia kitanzi alfajiri ya Jumatatu dakika chache tu  baada ya kuondoka nyumbani kwake kwenda kazini.

•Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Fredrick Ndunga alisema kwamba msimamizi huyo mwenye umri wa miaka 47 alijitoa uhai kwa kutumia kamba ya nailoni.

•Baadhi ya wakazi ambao hawakutaka kutajwa majina walidai kuwa msimamizi huyo alikuwa amekabiliwa na mizozo ya kinyumbani jambo ambalo lilimfanya kuwa mlevi.

meru
meru

Mshtuko na huzuni kubwa ziliwakumba wakazi wa eneo la Kahuro, kaunti ya Murang’a baada ya mwili wa chifu wao msaidizi kupatikana ukining'inia kwenye paa la ofisi yake.

Wakaazi waliokuwa wameenda kutafuta huduma katika afisi ya naibu chifu walishangaa kupata mwili wa Patrick Macharia ukining'inia juu ya paa.

Inadaiwa Macharia alijitia kitanzi alfajiri ya Jumatatu dakika chache tu  baada ya kuondoka nyumbani kwake kwenda kazini.

Kifo hicho kilisababisha shughuli katika kituo cha biashara cha Kahuro kusimama huku wakaazi wa eneo hilo wakimiminika katika afisi ya chifu baada ya kupokea habari hizo za kusikitisha.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Fredrick Ndunga alisema kwamba msimamizi huyo mwenye umri wa miaka 47 alijitoa uhai kwa kutumia kamba ya nailoni.

Ndunga alisema hawajabaini sababu zilizompelekea naibu chifu huyo kuchukua maisha yake. "Bado hatujajua ni nini kilimfanya chifu huyo kujitoa uhai na kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba alifanya hivyo katika ofisi yake," alisema kamishna huyo.

Ndunga alikariri kuwa watafanya uchunguzi kuhusu kujitoa mhanga akisema mwili huo ulitolewa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Muriranjas huku uchunguzi wa mwili ukisubiriwa.

Baadhi ya wakazi ambao hawakutaka kutajwa majina walidai kuwa msimamizi huyo alikuwa amekabiliwa na mizozo ya kinyumbani jambo ambalo lilimfanya kuwa mlevi.

Waliokuwa karibu na msimamizi huyo walidai kuwa chifu huyo msaidizi amekuwa akitishia kujitoa uhai bila kueleza masaibu anayopitia.

“Chifu wetu kwa muda wa miezi kadhaa amekuwa akikabiliwa na mizozo ya kinyumbani ambayo tunashuku kwamba ilimshinikiza kujitoa uhai. Lakini kazi ya uchunguzi tutawaachia maafisa wa usalama,” alidai mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

(Utafsiri: Samuel Maina)