Jinsi juhudi za wafungwa wa kigaidi za kuwasiliana na washirika wao baada ya kutoroka Kamiti zilidhalilishwa

Muhtasari

•Washukiwa walipofika katika mji wa Machakos walioga, wakapata kiamsha kinywa na wakanunua kofia tatu ili waweze kuficha nyuso zao wanapoendelea na safari.

•Mipango yao ilidhalilishwa wakati muuza duka ambaye waliendea awasaidie kuandikisha laini za simu alisita huku akidai watoe vitambulisho

Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi wakamatwa wakielekea Somalia
Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi wakamatwa wakielekea Somalia
Image: HISANI

Polisi wangali wanaendelea na uchunguzi  kuhusiana na tukio la wafungwa watatu wa kigaidi kutoroka kutoka jela ya Kamiti mnamo Novemba 15.

Kulingana na taarifa ambayo  ilitolewa na DCI usiku wa  Jumanne, uchunguzi wa awali umebaini washukiwa walipofanikiwa kutoka nje ya kuta za jela walijaribu kuwasiliana na washirika wao wa ugaidi wasiojulikana walipo.

Wapelelezi wa kupambana na ugaidi wamebaini kwamba washukiwa walipofika katika mji wa Machakos walioga, wakapata kiamsha kinywa na wakanunua kofia tatu ili waweze kuficha nyuso zao wanapoendelea na safari.

Baada ya matayarisho hayo washukiwa walinunua simu mbili ambazo walikusudia kutumia kuwasiliana na wenzao.

Hata hivyo mipango yao ilidhalilishwa wakati muuza duka ambaye waliendea awasaidie kuandikisha laini za simu alisita huku akidai watoe vitambulisho.

Imebainika washukiwa hata walijaribu kumhonga muuza duka huyo ili awasaidie kupata laini ila akasimama kidete na kukaidi ombi lao.

Katika taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii , DCI wamemsherehekea sana muuza duka huyo kwa kuweka nchi yake mbele badala ya pesa ambazo angefaidika nazo iwapo angekubali hongo ya washukiwa na awasaidie kuandikisha laini.