Polisi wakabiliana na majambazi waliovamia benki Kisumu

Muhtasari

•Timu ya maafisa walioongozwa na kamanda wa polisi katika  eneo la Nyanza, Karanja Muiruri wamekuwa wakishiriki vita ya risasi na majambazi hao ambao bado haijabainika ni wangapi kwa kipindi cha zaidi ya saa moja.

Polisi wakabiliana na majambazi waliovamia benki Kisumu
Polisi wakabiliana na majambazi waliovamia benki Kisumu
Image: DAN OGENDO

Polisi katika mji wa Kisumu wanaendelea kukabiliana na majambazi waliovamia benki ya Equity iliyo katika mtaa wa Ang'awa. 

Majambazi hao ambao wamejihami kwa bunduki wangali wamekatalia ndani ya benki hiyo.

Timu ya maafisa walioongozwa na kamanda wa polisi katika  eneo la Nyanza, Karanja Muiruri wamekuwa wakishiriki vita ya risasi na majambazi hao ambao bado haijabainika ni wangapi kwa kipindi cha zaidi ya saa moja.

"Lala chini!" sauti zingesikika huku wengine wakionekana kutii maagiza.

Majambazi wale wanasemekana kuvamia benki hiyo mwendo wa saa tano unusu. 

Wanafunzi watatu ambao walikuwa karibu na benki waliokolewa wakati milio ya risasi iliendelea kutanda hewani.

Walikimbizwa hospitalini na maafisa wa polisi. 

Baadhi ya wahudumu wa benki waliokuwa ndani wakati wa uvamizi huo pia wameokolewa.

Bado haijabainika iwapo kuna waliouawa katika uvamizi huo.

Inadaiwa majambazi walirusha vilipuzi vya machozi ili kuwatishia waliokuwa ndani ya benki.

Wazima moto wa kaunti ya Kisumu pia wameonekana katika eneo la tukio.