Hakuna pesa zilizoibwa wala aliyejeruhiwa wakati wa uvamizi wa benki Kisumu- Equity na Polisi watoa taarifa

Hakuna pesa zozote zilizoibiwa wakati wa uvamizi uliotokea Jumanne mwendo wa saa tano unusu mchana.

Muhtasari

•Katika taarifa yake, benki ya Equity imethibitishia Wakenya kwamba hakuna mfanyikazi wake aliyeangamia kwenye tukio hilo.

•Polisi walisema waliweza kuwatoa wateja wote na kuzuilia baadhi yao katika kituo cha polisi kwa uchunguzi zaidi

Polisi wakabiliana na majambazi waliovamia benki Kisumu
Polisi wakabiliana na majambazi waliovamia benki Kisumu
Image: DAN OGENDO

Benki ya Equity imetoa taarifa kufuatia tukio la jaribio la wizi ambalo lilitokea siku ya Jumanne katika tawi la Angawa, mjini Kisumu.

Katika taarifa yake, benki ya Equity imethibitishia Wakenya kwamba hakuna mfanyikazi wake aliyeangamia kwenye tukio hilo.

Equity pia imethibitishia wateja wake kuwa hakuna pesa zozote zilizoibiwa wakati wa uvamizi huo uliotokea mwendo wa saa tano unusu mchana.

"Tulikuwa na kisa ambapo majambazi waliojihami waliingia katika jumba la benki la Tawi letu la Kisumu Angawa. Maafisa wa usalama wakiongozwa na mamlaka za mitaa kwa sasa wako kwenye eneo la tukio. Wafanyakazi wote wako salama na hakuna pesa taslimu iliyopotea" Equity ilitangaza kupitia mitandao ya kijamii masaa machache baada ya uvamizi kuripotiwa.

Benki hiyo iliwaomba wateja wake katika tawi hilo kutumia njia mbadala za kupata huduma  kama vile tovuti na huduma za simu, ATM, na maajenti.

Polisi walisema walipokea taarifa kuhusu jaribio hilo la wizi kutoka kwa maafisa ambao walikuwa  katika zamu katika tawi hilo mwendo wa saa tano na dakika ishirini na tano.

Kulingana na polisi, inaaminika washukiwa walitishia mhudumu mmoja wa benki kupitia ujumbe wa  karatasi uliomwelekeza awapatie kiwango fulani cha pesa ambacho hakijathibitishwa.

Mhudumu huyo wa benki alitishika na tukio hilo likasababisha zogo katika benki hilo na hapo maafisa waliokuwa wameshika doria wakafunga benki na kuitisha usaidizi.

Polisi walisema waliweza kuwatoa wateja wote na kuzuilia baadhi yao katika kituo cha polisi kwa uchunguzi zaidi

Video za CCTV zitatumika kubaini iwapo kuna yeyote kati ya wateja waliozuliwa ambaye alihusika katika jaribio hilo la wizi.