Polisi aingia mitini baada ya kumpiga afisa mwenzake risasi Laikipia

Muhtasari

•Juhudi za kumkamata afisa huyo aliyekuwa akikimbia ziliambulia patupu baada ya kufanikiwa kutoroka huku akiwafyatulia risasi wenzake waliokuwa wanamfuata.

Bunduki
Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Polisi katika kaunti ya Laikipia wanamsaka mwenzao mmoja aliyeenda mafichoni baada ya kumpiga risasi na kumuua mwenzake katika kambi moja .

Konstebo Robert Longare alitoweka  na bunduki yake aina ya G3 iliyokuwa na risasi 20 baada ya kudaiwa kumpiga risasi na kumuua mwenzake John Siro walipokuwa kufuatia mzozo.

Juhudi za kumkamata afisa huyo aliyekuwa akikimbia ziliambulia patupu baada ya kufanikiwa kutoroka huku akiwafyatulia risasi wenzake waliokuwa wanamfuata.

Maafisa hao ni kutoka kitengo cha kupambana na wizi wa mifugo kilichopo Mteta farm. Wao ni miongoni mwa timu ya mashirika ya usalama yanayopambana na watu wenye silaha wanaoendesha shughuli zao kwenye ranchi za kibinafsi katika kaunti kubwa ya Laikipia.

Mwili wa afisa huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti huku msako wa afisa  aliyetoweka ukiendelea.

Kwingineko mmiliki wa bunduki mwenye leseni anatarajiwa kushtakiwa kwa mauaji baada ya mwathiriwa ambaye alimpiga risasi katika baa moja kando ya barabara ya Thika, Nairobi kufariki hospitalini miezi minne baadaye.

Mwathiriwa ambaye ni afisa wa polisi aliyetambulika kama Festus Musyoka alifariki hospitalini ambako amekuwa tangu Julai 2 alipopigwa risasi shingoni na mmiliki bunduki Dickson Mararo.

Tukio hilo lililotokea klabuni hapo baada ya mtu anayedaiwa kuwa ni mpenzi wa mwanamke mwenye umri wa ujana kugeuka kuwa ugomvi, na kusababisha kupigana risasi na kuwajeruhi watu watatu wakiwemo polisi wawili.

Majibizano hayo ya risasi yalihusisha raia mmoja mwenye bunduki, ambaye anadaiwa kuwapiga risasi watatu hao ambao baadaye walijisalimisha kwa polisi.

Bunduki ya Mararo, bastola aina ya  Glock, ilichukuliwa hadi kesi iamuliwe. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni pesa taslimu au bondi ya Sh10 milioni.

Hajamudu kuondoka kwa sababu dhamana ya pesa taslimu ilikuwa kubwa sana.Mahakama ilisikia kwamba Mararo, anayekabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua, aliwapiga risasi na kuwajeruhi waathiriwa wake watatu katika eneo la Quiver Lounge usiku wa Julai 2.

Upande wa mashtaka sasa unapanga kuboresha mashtaka hayo hadi ya mauaji.

(Utafsiri: Samuel Maina)