Jamaa akiri kuua mwanamke na kuelekeza polisi alikozika mwili

Muhtasari

•Ruto aliwaeleza wapelelezi alivyoua Veronica na kuacha mwili wake katika eneo la tukio kisha alfajiri iliyofuata akarudi pale akiwa amebeba jembe na kuchimbua kaburi ndogo ambamo alirusha mwili wa marehemu na kuuzika.

•Veronica ambaye alikuwa mfanyibiashara katika eneo la Mogotio alikosekana mnamo Novemba 12 baada ya kupigia mume wake, Marco Njuguna simu mida ya saa kumi na moja jioni akimuomba amtumie shilingi elfu tatu kwa dharura.

crime scene
crime scene

Wapelelezi katika kaunti ya Baringo wamefukua mwili wa mwanamke aliyeripotiwa kupotea katika hali tatanishi  wiki iliyopita.

Mwili wa Veronica Kanini (42)  ulipatikana ukiwa umezikwa katika kaburi lenye kina kifupi kando ya mto Molo ulio eneo la Mogoti baada ya mshukiwa mkuu katika mauaji hayo, Moses Kipichirchir Ruto (32) kukiri kutekeleza mauaji hayo na kuongoza wapelelezi hadi alikokuwa amezika mwili wa marehemu.

Hapo awali, Ruto ambaye alitiwa mbaroni mnamo Novemba 13 baada ya kuhusishwa na mauaji hayo alikuwa amekana kutekeleza kitendo hicho ila hatimaye alikiri matendo yake na kupeleka wapelelezi katika eneo la mauaji.

Alisimulia wapelelezi alivyoua Veronica na kuacha mwili wake katika eneo la tukio kisha alfajiri iliyofuata akarudi pale akiwa amebeba jembe na kuchimbua kaburi ndogo ambamo alirusha mwili wa marehemu na kuuzika.

DCI wamesema uchunguzi wa awali uliotekelezwa na wapelelezi wa uhalifu wa mitandaoni uliweka Ruto katika eneo la mauaji.

 

Njuguna alipouliza mkewe kwa nini alihitaji pesa zile alisikia sauti ya mwanaume ikimwagiza azungumze kwa Kiswahili.

Punde baada ya kupigia mumewe Veronica pia alipigia majirani wengine wawili ambao walimtumia kiasi cha pesa  ambacho hakijabainishwa.

Kufuatia hayo Njuguna ambaye tayari alikuwa amejawa na wasiwasi alifunga safari kuelekea Mogotio kusaka mke wake ila juhudi zake hazikufua dafu

Uchunguzi kuhusiana na kutoweka kwa marehemu uling'oa nanga na hapo wapelelezi kutoka makao kuu ya DCI wakasaidia kupata mshukiwa. 

Ruto alikamatwa baada ya wapelelezi kuvamia nyumba yake usiku wa Novemba 13.

Polisi walikuwa wameomba kuzuilia mshukiwa kwa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya manispa ya Nakuru huku uchunguzi wa mwili ukisubiriwa