Kamariny Stadium! ujenzi wa uwanja huo bado umekwama

Muhtasari

• Iten ni nyumbani kwa wanariadha wengi lakini eneo hilo halina uwanja wa kufanyia mazoezi.

• Wanariadha hao walisema kabla ya kazi ya ukarabati kuanza, walikuwa wakiutumia uwanja huo hata ukihitaji kufanyiwa ukarabati lakini kwa jinsi ulivyo kwa sasa hautumiki kabisa.   

•Kocha Ken Kibet alikuwa ametaka kujengwa kwa eneo la kukimbilia ili mafunzo yaendelee bila kukatizwa kazi ikiendelea.     

Wanariadha wameitaka serikali kukamilisha haraka ukarabati wa uwanja wa Kamariny ulioko Iten ili kuwawezesha kuwa na uwanja wa mazoezi.            

Naibu rais wa chama cha wanariadha nchini (AK) Paul Mutisya alisema inasikitisha kwamba Elgeyo Marakwet ni nyumbani mwa mabingwa wa riadha nchini na mahali ambapo wanariadha kutoka kote ulimwenguni wanapendelea kufanya mazoezi lakini hakuna kituo cha kawaida cha mazoezi.            

Akizungumza huko Iten, siku ya Alhamisi Mutisya alisema ukosefu wa vifaa vya kufanyia mazoezi umeua ndoto ya wanariadha wengi wanaochipuka na ambao hawawezi kumudu usafiri kila siku hadi chuo kikuu cha Eldoret katika kaunti jirani ya Uasin Gishu, uwanja wa karibu wa mazoezi wa umma unaopatikana kwa sasa.             

"Kwa wanariadha wa tajiriba wanaweza kumudu kutumia vifaa vya kibinafsi lakini inakuwa changamoto kwa wanariadha wanachipuka ambao wanategemea vifaa vya umma kufanya mazoezi," Mutisya alisema.            

Wakizungumza katika hafla hiyo, wanariadha mbalimbali walilalamika kuwa wakati ukarabati wa uwanja wa Kamariny ulipoanza, hawakupewa kituo mbadala cha kutumia wakati kazi zikiendelea.           

“Sasa kazi zimekwama, tumeachwa wenyewe huku wengi wetu wakilazimika kukimbia kando ya barabara tunapofanya mazoezi,” alisema mmoja wa wanariadha hao.            

Wanariadha hao walisema kabla ya kazi ya ukarabati kuanza, walikuwa wakiutumia uwanja huo hata ukihitaji kufanyiwa ukarabati lakini kwa jinsi ulivyo kwa sasa hautumiki kabisa.   

         Uwanja huo ulipangwa kufanyiwa ukarabati na idara ya michezo nchini kwa gharama ya Shilingi milioni 287. Ukarabati huo ulipaswa kuchukua miezi minane kuanzia Februari 2017.            

Kocha Ken Kibet alikuwa ametaka kujengwa kwa eneo la kukimbilia ili mafunzo yaendelee bila kukatizwa kazi ikiendelea.             

Hata hivyo, mkataba wa ujenzi wa uwanja huo ulisitishwa Januari mwaka huu kwa kushindwa kutimiza muda wa mkataba na mkataba mpya bado haujatolewa.