Mwanamke mwenye umri wa miaka 19 alijifungua mapacha walioungana katika hospitali ya Lenmek, eneo la Ogembo kaunti ya Kisii siku ya Jumatatu.
Daktari ambaye aliongoza shughuli ya kusaidia mwanadada huyo kujifungua, Evans Monda alisema mapacha hao wameunganishwa kuanzia kifuani hadi upande wa chini wa tumbo.
Vipimo vya mapema viliashiria viungo vingi vya watoto wale viko sawa.
Hata hivyo walihitajika kupelekwa katika hospitali ya hali ya juu ili waweze kutenganishwa.
Mapacha hao walizaliwa kupitia njia ya upasuaji ambao ulichukua takriban saa moja.
Mama ya mapacha hao, Lilian Moraa ambaye anatoka eneo la Kiong'ongi, Itumbe alifika hospitalini mwendo wa saa tano usiku wa kuamkia Jumanne baada ya kutumwa pale kutoka hospitali ya Ogembo Level 4.
Alisema kujifungua huko kwake kwa kwanza kulikuwa kwa kushangaza.
Alisema alipata uchungu wa leba Jumapili mwendo wa saa kumi na mbili.
Alikimbizwa katika hospitali ya Ogembo kabla ya kutumwa hospitali ya kibinafsi ya Lenmek kufuatia matatizo.
Dkt Monda alisema jambo kama lile lilikuwa la kwanza kuonekana pale.
"Kesi kama zile si za kawaida.." Alisema.
Kutenganisha mapacha walioungana mara nyingi ni utaratibu unaohitaji upangaji wa makini na wa kina pamoja na kuhusisha wataalamu wengi.
(Utafsiri: Samuel Maina)