Mwanamume apatikana na hatia ya kumnajisi msichana Loitoktok

Muhtasari

• Mwanamume mwenye umri wa miaka 28 amepatikana na hatia ya kumnajisi msichana wa miaka 17 na mahakama ya Loitoktok.   

• Msichana huyo aliondoka nyumbani kwao bila kuwajulisha wazazi wake na kwenda nyumbani kwa mshtakiwa ambapo alikaa kwa siku nne. 

• Mahakama iliambiwa kwamba msichana huyo alituma ujumbe mfupi kwa mamake kwa kutumia simu ya mshtakiwa akimjulisha kuwa alikuwa na mshtakiwa. 

Mahakama
Mahakama

Mwanamume mwenye umri wa miaka 28 amepatikana na hatia ya kumnajisi msichana wa miaka 17 na mahakama ya Loitoktok.            

Benjamin Mutuku ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Caroline Ndumia alishtakiwa kuwa tarehe tofauti kati ya Januari 4 hadi 7, 2020 katika eneo la Olchoro huko Loitoktok alimnajisi msichana huyo. 

Msichana huyo hapo awali aliambia mahakama jinsi mnamo Januari 3, alikutana na mshtakiwa ambaye alikuwa akimfahamu kwa muda mrefu na kumwomba aende kuishi naye kama mke wake. 

Msichana huyo aliondoka nyumbani kwao bila kuwajulisha wazazi wake na kwenda nyumbani kwa mshtakiwa ambapo alikaa kwa siku nne. 

Mahakama ilisikia kwamba babake msichana huyo, Kennedy Suryanag, aliripoti katika kituo cha polisi cha Kimana kwamba bintiye alitoweka alipokosa kufika siku moja baada ya kutoweka kwake.

Mahakama iliambiwa kwamba msichana huyo alituma ujumbe mfupi kwa mamake kwa kutumia simu ya mshtakiwa akimjulisha kuwa alikuwa na mshtakiwa. 

Maafisa wa polisi walifuatilia simu ya mshtakiwa hadi nyumbani kwake ambapo waliwapata wawili hao. 

Mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Olchoro ambako alishtakiwa kwa kosa hilo huku msichana huyo akipelekwa katika hospitali ndogo ya Loitoktok ambapo ilithibitishwa alikuwa amenajisiwa. 

Katika utetezi wake mshtakiwa alikana kumnajisi mtoto huyo na kuongeza kuwa alikuwa hajawahi kumuona.

Aliambia mahakama kuwa alikamatwa akiwa anafanya biashara ya uchuuzi na kupelekwa hadi kituo cha polisi na kufunguliwa mashtaka ya unajisi. 

Hata hivyo, mahakama iliamua kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha madai dhidi ya mshukiwa.  Atahukumiwa Desemba 6, 2021.