DCI Kinoti amsherehekea dereva aliyeripoti wanafunzi waliokuwa wanavuta bangi na kulewa ndani ya matatu

Muhtasari

•Kinoti alimkaribisha Muthoni ofisini mwake jioni ya Alhamisi kufuatia mwaliko ambao alimpatia baada ya ripoti kuhusu kufutwa kazi kwake kuenea.

•Kinoti alimsherehekea Muthoni kwa ujasiri ambao alionyesha huku akilaani kutimuliwa kwake kazini.

•Kinoti alihimiza Muthoni aendelee kushikilia maadili yake ya kusimama na kilicho sawa bila kujali kama kwamba kinahatarisha kazi yake. 

DCI Kinoti akutana na dereva John Maina na MCA Mercy Nungari katika ofisi za Mazingira Complex jioni ya Alhamisi
DCI Kinoti akutana na dereva John Maina na MCA Mercy Nungari katika ofisi za Mazingira Complex jioni ya Alhamisi
Image: TWITTER// DCI

Hatimaye bosi wa DCI George Kinoti alikutana na dereva John Maina Muthoni ambaye aliripoti wanafunzi waliokuwa wanatumia mihadarati ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha takriban wiki mbili zilizopita.

Kinoti alimkaribisha Muthoni ofisini mwake jioni ya Alhamisi kufuatia mwaliko ambao alimpatia baada ya ripoti kuhusu kufutwa kazi kwake kuenea.

Muthoni anadaiwa kupoteza kazi yake ya dereva katika kampuni ya usafiri ya 2NK baada ya kuripoti wanafunzi 7 wa kiume na 7 wa kike ambao walikuwa wanavuta bangi na kubugia vile ndani ya matatu walipokuwa wanasafiri kuenda nyumbani kwa kipindi cha likizo fupi.

Dereva huyo alielekea kituoni baada ya wanafunzi wale kumpatia vitisho alipowaonya dhidi ya kutumia mihadarati ile.

Kinoti alimsherehekea Muthoni kwa ujasiri ambao alionyesha huku akilaani kutimuliwa kwake kazini.

Alikashifu kuongezeka kwa utumizi wa madawa ya kulevya miongoni mwa wanafunzi  huku akisema kumechangia kuharibika kwa maisha ya vijana wengi nchini.

Kinoti alihimiza Muthoni aendelee kushikilia maadili yake ya kusimama na kilicho sawa bila kujali kama kwamba kinahatarisha kazi yake. 

Muthoni alikuwa ameandamana na mwakilishi wadi  wa kuteuliwa Mercy Nungari.

Hivi majuzi gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alimpatia Muthoni kazi ya dereva katika kitengo kimoja cha kaunti hiyo.