Polisi wachunguza kifo cha jamaa aliyepatikana amefariki ndani ya gari Narok

Muhtasari

•Kamanda wa polisi kaunti ya Narok Kizito Mutoro alisema polisi walikuwa wanaitika mayowe kutoka kwa raia waliofika katika eneo la tukio wakati walipata mwili wa James Mukami ndani ya gari huku ukiwa na jeraha kubwa la kisu chini ya kwapa la kushoto.

Crime scene photo
Crime scene photo

Polisi katika kaunti ndogo ya Narok Kaskazini wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 36 ulipatikana ukiwa kwenye gari aina ya Isuzu D-max katika kituo cha biashara cha Ewaso Nyiro Ijumaa usiku.

Kamanda wa polisi kaunti ya Narok Kizito Mutoro alisema polisi walikuwa wanaitika mayowe kutoka kwa raia waliofika katika eneo la tukio wakati walipata mwili wa James Mukami ndani ya gari huku ukiwa na jeraha kubwa la kisu chini ya kwapa la kushoto.

Bosi huyo wa polisi alisema kulingana na ripoti za awali, dereva wa Isuzu D-max nambari ya usajili KCV 180Z kwa jina David Kamau, 31, alikuwa ameenda kuwinda pamoja na marehemu katika eneo la Narosura huko Narok kusini ambapo kwa bahati mbaya alimdunga kisu.

Hata hivyo, mwanaume huyo alifariki dunia akiwa njiani alipokuwa akimkimbiza hospitalini na kumlazimu dereva wa gari hilo kusimama nyumbani kwa marehemu ili kumjulisha mkewe kuhusu tukio hilo.

Mke wa marehemu alipiga nduru kali na kusababisha wananchi kufika pale nyumbani kwao, ambapo walimkuta marehemu akiwa amefariki ndani ya gari.

Bosi huyo wa polisi alisema dereva wa gari hilo ambaye ndiye mshukiwa mkuu alikamatwa huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Narok kuhifadhiwa.

Kisa hicho kinajiri siku mbili baada ya mwili wa kijana wa miaka 24 kupatikana ukiwa katika kituo cha afya cha Siyiapei majira ya asubuhi ukiwa na majeraha mabaya kichwani.

(Utafsiri: Samuel Maina)