Wateketezaji washambulia tena na kuchoma nyumba ya mwanamke mkongwe aliyeuawa kwa madai ya uchawi Kisii

Muhtasari

•Nyumba ya Jemima Mironga ilikuwa imechomwa tena mwezi uliopita na baadae ikafanyiwa ukarabati kupitia usaidizi wa wanaharati wa kutetea haki za binadamu katika kaunti hiyo.

•Naibu kamishna wa kaunti Patrick Muriira alisema hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo la moto ila mali yenye thamani isiyojulikana  iliharibiwa.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Watu wasiojulikana wameteketeza nyumba ya mmoja wa wanawake wakongwe ambaye aliuawa kufuatia madai ya uchawi katika eneo la Kitutu Chache Kaskazini, kaunti ya Kisii zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Nyumba ya Jemima Mironga ilikuwa imechomwa tena mwezi uliopita na baadae ikafanyiwa ukarabati kupitia usaidizi wa wanaharati wa kutetea haki za binadamu katika kaunti hiyo.

Wanaharakati hao pia walikuwa wamejengea watoto wa Mironga nyumba ingine moja pale.

Kufikia jioni ya Jumatatu police katika eneo la Rioma bado hawakuwa wamebaini kilichopelekea uchomaji ule.

Naibu kamishna wa kaunti Patrick Muriira alisema hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo la moto ila mali yenye thamani isiyojulikana  iliharibiwa.

Janet Moraa ambaye ni binti wa marehemu Mironga alisema waligundua moto huo mwendo wa saa tano usiku ila juhudi za kuuzima zikagonga mwamba kwani ulikuwa unaenea haraka.

"Tulikuwa tumelala tayari ila kwa neema yake Mungu tulinusurika kifo" Moraa alisema.

Uteketezaji huo unaonekana kuhusiana na tukio la mwezi jana ambapo wanawake wanne wakongwe ikiwemo Mironga waliuawa kwa madai ya kuteka nyara mwanafunzi wa shule ya upili usiku.

Mwanafunzi huyo alipatikana akiwa amezuzua nje ya nyumba yake asubuhi iliyofuata.

Moraa aliomba ulinzi kutoka kwa serikali kufuatia tukio hilo huku akidai maisha ya familia yao yalikuwa hatarini.

Muriira alisema polisi wameanzisha uchunguzi.

(Utafsiri: Samuel Maina)