Jamaa aliyevalia sare za kijeshi avamia kituo cha polisi na kuhangaisha afisa wa kike Kisii

Muhtasari

•Onderi alimshtumu konstabo Maina kwa kutovaa sare rasmi ya polisi kabla ya kumvuruta kutoka eneo lake la kazi kwa nguvu. 

George Onderi
George Onderi
Image: TWITTER/ DCI

Polisi katika kaunti ya Kisii wanazuilia jamaa mmoja anayeripotiwa kuingia katika kituo cha polisi cha Suneka akiwa amevalia koti la kijeshi na kuhangaisha afisa wa kike usiku wa Jumatatu.

George Onderi 27, aliwasili kituoni mwendo wa saa tatu usiku kwa gari lake aina ya Toyota Belta na kufululiza moja kwa moja hadi kwa meza ya kupigia ripoti ambapo alimpata afisa Mary Maina na kuanza kumhangaisha.

Onderi alimshtumu konstabo Maina kwa kutovaa sare rasmi ya polisi kabla ya kumvuruta kutoka eneo lake la kazi kwa nguvu. 

Kizaazaa kile kilivutia polisi wengine ambao walikimbia katika eneo la tukio kumsaidia mwenzao.

Mshukiwa anaripotiwa kukataa kujitambulisha alipoagizwa na naibu OCS wa Suneka Cephas Ombija. 

Kufuatia hayo mshukiwa aliwekwa kizuizini huku polisi wakianza  uchunguzi kubaini iwapo amehusika katika uhalifu wowote eneo hilo.

Onderi atashtakiwa kwa makosa ya uigaji na kusababisha fujo.