Mzee aua mwanawe aliyerejea nyumbani baada ya miaka 4 akiwa mlevi chakari

Muhtasari

•James Tarus 73, anadaiwa kumpiga kichwa mwanawe kutumia mbao iliyokuwa karibu kisha kumfunga kamba shingoni  na kumzuilia kwenye sofa mwendo wa saa moja usiku wa Jumapili katika eneo la Chepsiro.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Trans Nzoia wanazuilia mwanamume mmoja anayeripotiwa kushambulia mwanawe wa miaka 31 hadi kifo kwa kukatiza usingizi wake.

James Tarus 73, anadaiwa kumpiga kichwa mwanawe ambaye hajaonekana pale nyumbani katika kipindi cha miaka minne ambacho kimepita kutumia mbao iliyokuwa karibu mwendo wa saa moja usiku wa Jumapili katika eneo la Chepsiro.

Baada ya kumgonga kichwa, mshukiwa anaripotiwa kumfunga mwanawe kamba shingoni  na kumzuilia kwenye sofa.

Kulingana na DCI, marehemu alikuwa amepitia kwa baa na kubugia chupa kadhaa za mvinyo kabla ya kuelekea nyumbani na kupata babake akiwa amelala.

Baada ya kufika pale marehemu alienda hadi chumba cha babake na kumuamsha. Mzee huyo aliamka akiwa amejawa na ghadhabu na ndipo akamshambulia mwanawe.

Chifu wa eneo hilo aliandamana na majirani kadhaa na kupata mwili wa jamaa huyo ukiwa umefungwa kwa kiti.

Tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Cherangany na mshukiwa ambapo mshukiwa anazuiliwa akisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.