Polisi akamatwa akiwa amejificha kwa mpenzi wake baada ya kuua afisa mwenzake Naivasha

Muhtasari

•Koplo Joseph Muthunga anazuiliwa katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa siku ya Jumapili akiwa amejificha katika nyumba ya mpenziwe mjini Nakuru.

•Walioshuhudia walisema Polo alimuuliza mshukiwa kwa nini alikuwa mlevi ilhali alipaswa kuwa kazini, jambo ambalo lilimkasirisha akachukua bunduki na kumuua papo hapo.

•Idara ya polisi imelaani vikali mauaji yaliyotekelezwa na Muthunga huku ikifariji familia ya marehemu.

Pingu
Image: Radio Jambo

Afisa aliyetoroka baada ya kumpiga risasi na kumuua bosi wake kufuatia mabishano katika kambi ya Kedong iliyo Naivasha, Kaunti ya Nakuru hatimaye alitiwa mbaroni.

Koplo Joseph Muthunga anazuiliwa katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa siku ya Jumapili akiwa amejificha katika nyumba ya mpenziwe mjini Nakuru.

Muthunga alikuwa amejificha pale tangu usiku wa Jumamosi baada ya kushtumiwa kwa kuua sajenti mkuu Ayub Polo wakiwa kambini.

Mshukiwa alikuwa ameficha bunduki yake mahali kwingine na baadae aliongoza polisi hadi pale kuichukua.  Bunduki hiyo ilikuwa na risasi 25.

Polisi walisema mshukiwa na marehemu walikuwa miongoni mwa maafisa waliohudhuria karamu ya Krismasi wakati mabishano yalipozuka.

Walioshuhudia walisema Polo alimuuliza mshukiwa kwa nini alikuwa mlevi ilhali alipaswa kuwa kazini. Jambo hili lilimkasirisha Muthunga ambaye alichukua bunduki yake aina ya G3,  akampiga Polo risasi kwa karibu na kumuua papo hapo.

Baadaye alitoroka kutoka kambini na inasemekana alifuatiliwa hadi mji wa Nakuru takriban kilomita 50.

Wenzake waliokuwepo walikimbilia usalama wao waliposikia milio ya risasi na wakati walipokuwa wanarudi mshukiwa tayari alikuwa ametoweka.

Polisi walisema atahojiwa ili kubaini nia yake.

Mkuu wa polisi katika eneo la Bonde la Ufa Fredrick Ochieng alisema walimkamata afisa huyo bila kushuhudia upinzani wowote.

Idara ya polisi imelaani vikali mauaji yaliyotekelezwa na Muthunga huku ikifariji familia ya marehemu. Mshukiwa atashtakiwa baada ya uchunguzi kukamilika.