Majambazi wapatia mbwa sumu, wafunga walinzi kisha kuiba pesa na vito vya thamani Muthaiga

Ulinzi umeimarishwa katika eneo hilo ili kupunguza matukio ya ujambazi.

Muhtasari

•Polisi walisema genge hilo lilielekea nyumbani kwa Patel mwendo wa saa kumi na moja asubuhi wakashika familia hiyo mateka na kuwaibia Sh150,000, vito na saa zenye thamani ya Sh1.7 milioni.

•Mkuu wa polisi katika eneo la Starehe Julius Kiragu alisema genge hilo linaonekana kuwa na taarifa za ndani na msako wa kuwakamata unaendelea.

crime scene
crime scene

Genge la majambazi lilimpa mbwa sumu, likawafunga walinzi na kushikilia mateka familia moja katika boma mbili eneo la Muthaiga, Nairobi.

Genge hilo la takriban wanaume watatu ambalo lilikuwa limejihami kwa silaha mbalimbali ikiwemo   bastola liliendelea kuingia kwa nyumba hizo na kuiba vifaa vya elektroniki, vito vya thamani na pesa taslimu.

Polisi walikuwa wanachunguza wizi katika manyumba ya Ken Odede na Haren Patel siku ya Jumapili, Boxing Day.

Wezi hao walikata uzio wa 'kayapple' na ule wa umeme katika makazi ya Odede, wakamtilia mbwa sumu na kuwafunga walinzi wake kutoka kwa kikundi cha usalama cha kibinafsi.

Walikaa pale kwa muda. Kwa wakati huo mwenye boma pamoja na familia yake walikuwa wametoka, polisi na wahasiriwa walisema.

Mtunza bustani aliyekuwa anaripoti kazini aliwakuta walinzi wakiwa wamefungwa kwenye chumba kimoja na kuwaita polisi.

Polisi walisema genge hilo lilielekea nyumbani kwa Patel mwendo wa saa kumi na moja asubuhi wakashika familia hiyo mateka na kuwaibia Sh150,000, vito na saa zenye thamani ya Sh1.7 milioni.

Genge hilo liliwaamuru watu wawili familia hiyo kuwabeba kwa gari la familia kutoka pale hadi barabara kuu ya Thika ambapo walishuka. Walimwambia dereva arudi nyumbani huku wakiondoka.

Mkuu wa polisi katika eneo la Starehe Julius Kiragu alisema genge hilo linaonekana kuwa na taarifa za ndani na msako wa kuwakamata unaendelea.

"Isipokuwa kuuawa kwa mbwa kutumia sumu, hakuna mtu aliyejeruhiwa. Tutawapata," Kiragu alisema.

Alisema wameongeza ulinzi katika eneo hilo ili kupunguza matukio ya ujambazi.

Visa vya wizi na wizi vinazidi kuongezeka katika eneo hilo.  Eneo hilo ni mojawapo ya maeneo yenye ulinzi mkali katika jiji hilo.

Polisi wanashauri wamiliki wa nyumba kuwachunguza wafanyikazi wao kila wakati ili kuepuka matukio kama hayo.

Mamlaka pia inashauri dhidi ya kuweka kiasi kikubwa cha pesa na vito vya thamani nyumbani