Jamaa aliyekiri kuua 'mpenziwe' aongoza polisi hadi alikozika mkewe na mwanawe baada ya kukiri kuwaua pia

Muhtasari

•Kufuatia mahojiano ya masaa mengi mnamo Desemba 26, mshukiwa alikiri kumuua mpenzi wake Purity Chebet 24, na mtoto wake Ezra ambaye alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.

•Ruto ambaye alikuwa amemuoa Chebet alisema alitekeleza mauaji hayo kufuatia mzozo wa kinyumbani.

•Wapelelezi wanaamini kuwa mshukiwa huyo ametekeleza mauaji zaidi wanatafuta makaburi mengine huku mshukiwa akitarajiwa kusomewa mashtaka mnamo Januari 21, 2022.

Image: TWITTER// DCI

Jamaa mmoja ambaye alikamatwa takriban mwezi mmoja uliopita kufuatia mauaji ya kikatili ya mfanyibiashara Veronica Kanini jana aliongoza wapepelelezi hadi kwa makaburi mengine mawili ambapo alikuwa amewazika wahasiriwa wake wengine.

Kulingana na DCI, Muuaji huyo Moses Kipchirchir Ruto, 34, aliongoza wapelelezi kutoka kituo cha Mogotio hadi kwenye makaburi mawili ya kina kirefu ambapo alikuwa amemzika mwanamke anayeaminika kuwa mkewe na mwanawe.

Ruto alikiri kutekeleza mauaji hayo baada ya kuhojiwa na wapelelezi ambao waliamini Kanini hakuwa mhasiriwa wake wa pekee.

Kufuatia mahojiano ya masaa mengi mnamo Desemba 26, mshukiwa alikiri kumuua mpenzi wake Purity Chebet 24, na mtoto wake Ezra ambaye alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.

Alisema aliwaua mapema mwezi Septemba na kuzika mili yao  kwenye kingo za Mto Molo katika eneo la Mogotio, mita chache kutoka mahali ambapo alimzika Kanini baadae.

Ruto ambaye alikuwa amemuoa Chebet alisema alitekeleza mauaji hayo kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Siku ya Jumatatu aliongoza wapelelezi hadi alikozika miili ya aliyekuwa mkewe pamoja na mwanawe mchanga..

Baada ya eneo hilo kuchimbwa mabaki ya mama na mtoto ambayo yalikuwa yameoza  yalipatikana.

Inaaminika muuaji huyo alikuwa kwenye mahusiano ya siri na Kanini kabla yao kutofautiana baada ya marehemu kumwambia kuwa amepata mwanamume mwingine. Kufuatia hayo Ruto akaamua kumuangamiza.

Wapelelezi wanaamini kuwa mshukiwa huyo ametekeleza mauaji zaidi wanatafuta makaburi mengine huku mshukiwa akitarajiwa kusomewa mashtaka mnamo Januari 21, 2022.