"Madaktari wanasema atasalia kitandani mwezi mmoja" DP Ruto atoa taarifa kuhusu afya ya Itumbi

Muhtasari

•Ruto amethibitisha alimtembelea mtaalamu huyo wake wa masuala ya kidijitali na kumpata akiwa imara na mchangamfu.

•Amesema alimpata mwanablogu huyo akiwa amefungwa bandeji kwenye mkono wake na miguu kutokana na mateso aliyopitia mikononi mwa watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama.

Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Image: TWITTER// WILLIAM RUTO

Naibu rais William Ruto ametoa taarifa kuhusu ziara yake ya hospitalini Jumanne jioni kumfariji mwanablogu Dennis Itumbi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ruto amethibitisha alimtembelea mtaalamu huyo wake wa masuala ya kidijitali na kumpata akiwa imara na mchangamfu.

Hata hivyo, naibu rais amefichua kwamba madaktari walimuarifu kuwa Itumbi angebaki amelazwa kitandani kwa muda wa mwezi mmoja.

"Walitaka kuua roho yake lakini DI ana nguvu na amechangamka ingawa madaktari wanasema atasalia kitandani kwa mwezi mmoja" Ruto amesema.

Ruto amesema alimpata mwanablogu huyo akiwa amefungwa bandeji kwenye mkono wake na miguu kutokana na mateso aliyopitia mikononi mwa watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama.

Naibu rais amelaani vikali mateso aliyofanyiwa Itumbi huku akihakikishia Wakenya kuwa hivi karibuni watakombolewa kutoka kwa  minyororo ya unyanyasaji.

"Nilikaa na Comrade DI jana jioni, niliona mkono na miguu yake ikiwa imefungwa bandeji sana, matokeo ya kuteswa na watu ambao walipaswa kuwa pale ili kumlinda yeye na sisi sote. Sasa wamegeuka kuwa wenye vurugu na wabaya baada ya simulizi, vitisho na usaliti dhidi yetu imeshindwa" Ruto alisema.

"Kama Denis, sote lazima tuwe na nguvu tukijua miezi michache ijayo tutashinda hali ya kutokujali, haki, kiburi na madharau na kuliweka taifa letu kwa wema" Aliongeza.

Jioni ya Jumanne jioni naibu rais alifika katika hospitali ya  Nairobi West kumuona mwanablogu Dennis Itumbi ambaye amelazwa pale.

Katika ukurasa wake wa Twitter Ruto alipakia picha kadhaa zilizoonyesha akishiriki gumzo na mwanablogu huyo ambaye alionekana akiwa amefungwa mifereji kwenye mapua na alikuwa na  plasta mkononi na mguuni.

"Pole Dennis. Pona haraka. Mungu ni Mwenyezi." Ndio ulikuwa ujumbe wa naibu rais kwa Itumbi.

Mwanablogu huyo na ambaye ni mtaalamu wa naibu rais wa masuala ya kidigitali alipelekwa hospitalini Ijumaa wiki iliyopita.

Itumbi alitekwa nyara mnamo Alhamisi na kupigwa kabla ya kutelekezwa kando ya barabara akiwa uchi katika eneo la Lucky Summer, Kasarani.

Alikuwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wakati alipatikana na dereva wa teksi. Alipelekwa hospitalini Ijumaa asubuhi.

Baadae alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kukabiliwa na matatizo ya Pneumonia.

Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Image: TWITTER// WILLIAM RUTO