{+Picha} Naibu Rais William Ruto amtembelea mwanablogu Itumbi hospitalini kumfariji

Muhtasari

•"Pole Dennis. Pona haraka. Mungu ni Mwenyezi." Ndio ulikuwa ujumbe wa naibu rais kwa Itumbi.

Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Ruto amtembelea Itumbi hospitalini kumfariji
Image: TWITTER// WILLIAM RUTO

Jioni ya Jumanne jioni naibu rais William Ruto alifika katika hospitali ya  Nairobi West kumuona mwanablogu Dennis Itumbi ambaye amelazwa pale.

Katika ukurasa wake wa Twitter Ruto alipakia picha kadhaa zilizoonyesha akishiriki gumzo na mwanablogu huyo ambaye alionekana akiwa amefungwa mifereji kwenye mapua na alikuwa na  plasta mkononi na mguuni.

"Pole Dennis. Pona haraka. Mungu ni Mwenyezi." Ndio ulikuwa ujumbe wa naibu rais kwa Itumbi.

Mwanablogu huyo na ambaye ni mtaalamu wa naibu rais wa masuala ya kidigitali alipelekwa hospitalini Ijumaa wiki iliyopita.

Itumbi alitekwa nyara mnamo Alhamisi na kupigwa kabla ya kutelekezwa kando ya barabara akiwa uchi katika eneo la Lucky Summer, Kasarani.

Alikuwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wakati alipatikana na dereva wa teksi. Alipelekwa hospitalini Ijumaa asubuhi.

Baadae alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kukabiliwa na matatizo ya Pneumonia.

Itumbi amekuwa mwiba kwa viongozi wakuu serikalini, ambao baadhi yao amewataja kuwa wezi wa ardhi. Amekuwa akimwita askari polisi mkuu "kikaragosi" na kuwatambulisha walengwa wake kwenye mitandao ya kijamii.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema wanachunguza tukio hilo.