Ngumi na mateke Bungeni huku wabunge wakipigia kura muswada wa UhuruRaila

Muhtasari

•Bunge hilo liligeuka kuwa ulingo wa ndondi huku hasira zikipamba moto mara baada ya kikao cha alasiri kurejea huku wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wakilalamika

•Mbadi anasemekana kumpiga Koros usoni baada ya mbunge huyo mshirika wa UDA kuenda kukabiliana naye wakati wabunge walikuwa wakipiga kura  kuhusu marekebisho yaliyowasilishwa na mbunge wa Kandara Alice Wahome.

•Omulee pia aliwataja na kuwaonya mbunge mteule David Sankok na John Kiarie kwa kuwarushia wenzao chupa za maji na kuwasumbua.

Kiongozi wa wachache John Mbadi akionyesha kidole chake baada ya kuzozana na Mbunge wa Sigowet/Soin Kipsemgeret Koros
Kiongozi wa wachache John Mbadi akionyesha kidole chake baada ya kuzozana na Mbunge wa Sigowet/Soin Kipsemgeret Koros
Image: LUKE AWICH

Siku ya Jumatano vita vya ngumi na mateke bungeni  vilitatiza shughuli ya upiga kura muhimu wa wabunge kuhusu muswada wa muungano unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Kiongozi wa walio wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi alisimamishwa kuhudhuria vikao vitano mfululizo vifuatavyo kwa kumpiga ngumi na kumjeruhi Mbunge wa Sing'owet-Soin Kipsengeret Koros.

Spika wa muda Chris Omulele ambaye ni mbunge wa Luanda aliamuru kwamba Mbadi alikuwa amekiuka Kanuni za Kudumu za Bunge kwa kuhusika katika vita vya ngumi.

"Lazima kuwe na utaratibu katika Bunge hili," aliamuru Omulele huku akimuagiza Mbadi atoke nje ya eneo la bunge mara moja.

Spika alilazimika kutumia Kanuni za Kudumu za Bunge kuwaadhibu wabunge wakorofi baada ya kukaidi amri ya kurejea vikao vyao.

"Utulivu! Hamuwezi kuwa mmesimama wakati mwenyekiti amesimama," Omulele aliwaelekeza mara kwa mara wabunge waliojazana eneo la rungu ya bunge (mace)

Wabunge wa Tangatanga wanaomuunga mkono Ruto walikuwa wamesimama kuzunguka meza moja, na hivyo kuzua mtafaruku huku wabunge wanaounga mkono rais Kenyatta na Raila Odinga  wakiwakabili.

Kwa wakati mmoja wabunge wengi zaidi walirekodiwa na wenzao wakipigana ngumi kwenye pale bungeni lakini spika hakuwaona.

Mrengo wa naibu rais ulikuwa umekusanya wabunge 136 ndani ya Bunge katika karata ya nambari dhidi ya vikosi vilivyojumuishwa vya Uhuru na Raila ambao walikuwa na wabunge 153.

Naibu rais alikuwa amekusanya wabunge wake pamoja chini ya uongozi wa Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale.

Mbadi anasemekana kumpiga Koros usoni baada ya mbunge huyo mshirika wa UDA kuenda kukabiliana naye wakati wabunge walikuwa wakipiga kura  kuhusu marekebisho yaliyowasilishwa na mbunge wa Kandara Alice Wahome.

Kulikuwa na mtafaruku uliodumu kwa muda wa saa moja wabunge walipozozana kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya muswada wa marekebisho ya vyama vya Kisiasa ya 2021 yaliyokabiliwa na utata.

Bunge hilo liligeuka kuwa ulingo wa ndondi huku hasira zikipamba moto mara baada ya kikao cha alasiri kurejea huku wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wakilalamika.

Omulele alilazimika kusimamisha kikao hicho kwa dakika 15 kwa wakati mmoja ili kuwatuliza wabunge.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusimamishwa kuhudhuria  vikao vitano vya bunge, Mbadi ambaye alikiri kumpiga ngumi mbunge wa Sigowet/Soin alikashifu uamuzi wa Spika huku akisema ni kinyume na kanuni za bunge.

Kulingana na Mbadi, Koros alikuwa akisisitiza kumpigia kura mwanachama ambaye hayupo licha ya maonyo kadhaa dhidi ya hatua hiyo ya makarani.

“Nilipomwambia (Koros) aondoke ndipo alinigeukia na kweli aliniuma kidole,” Mbadi alisema akinyooshea kidole chake cha shahada kilichofungwa.

"Nilikuwa najilinda" Alisema.

Kiongozi huyo wa Wachache hata hivyo alionyesha imani kuwa upande wake bado ungeshinda marekebisho ya mrengo wa Tangatanga ambayo yalilenga kutatiza kupitishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa wa 2021.

Omulee pia aliwataja na kuwaonya mbunge mteule David Sankok na John Kiarie kwa kuwarushia wenzao chupa za maji na kuwasumbua.

Alitaja matukio ya Jumatano kuwa ya kufedhehesha na ya kuvunja moyo.

"Inavunja moyo na kufedhehesha kwa wanachama kuwa na tabia kama hii," Mbunge wa Luanda alisema.

Wabunge wa Ruto walikuwa wamejaribu kuzorotesha mjadala kuhusu mswada huo kwa kufanya marekebisho kadhaa na kufanya isiwezekane kuhitimisha mswada huo.

Upande wa Ruto ulionekana kufurahia idadi kubwa katika Ikulu kabla ya mambo kubadilika na kupendelea timu ya Uhuru-Raila.