Pigo kwa Mudavadi baada ya Savula kumtema na kumuunga mkono Raila Odinga

Muhtasari

•Mbunge huyo alisema kinyang’anyiro cha urais 2022 kitakuwa ni mbio za farasi wawili kati ya Raila na Naibu Rais William Ruto.

•Hata hivyo alifafanua kuwa bado angali mwanachama wa ANC ambacho alitumia kuingia bungeni.

Mbunge wa Lugari Ayub Savula akiwa nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa Afya Joshua Angatia katika eneo bunge la Malava
Mbunge wa Lugari Ayub Savula akiwa nyumbani kwa aliyekuwa waziri wa Afya Joshua Angatia katika eneo bunge la Malava
Image: HILTON OTIENO

Naibu kiongozi wa chama cha ANC na ambaye ni mbunge wa Lugari Ayub Savula amemtema rasmi Musalia Mudavadi na kumuunga mkono Raila Odinga kuwa rais.

Mbunge huyo alisema kinyang’anyiro cha urais 2022 kitakuwa ni mbio za farasi wawili kati ya Raila na Naibu Rais William Ruto.

Mbunge huyo mwenye ushawishi mkubwa katika eneo la Magharibi na ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Musalia, alitangaza kwamba pia amesitisha mazungumzo yoyote na Muungano wa One Kenya.

Mbunge huyo hata hivyo alifafanua kuwa bado angali mwanachama wa ANC ambacho alitumia kuingia bungeni.

"Sijahama ANC lakini leo nimejiunga rasmi na Azimio La Umoja," alisema Savula.

Mbunge huyo alizungumza katika mkutano ulioandaliwa katika uwanja wa Bukhungu ambapo viongozi wa Magharibi mwa Kenya wakiongozwa na katibu mkuu wa Cotu Francis Atwoli walifanya mkutano wa Azimio La Umoja.

"Pia nimeachana na muungano wa One Kenya, nimechoshwa na upuuzi huo," Savula alisema.

Hatua  ya Savula ni pigo kubwa kwa Musalia katika juhudi zake za kudhoofisha ushawishi wa kisiasa wa Raila na kuunganisha eneo lake la magharibi.

"Mashindano ya urais 2022 ni ya mbio za farasi wawili kati ya Raila na Ruto, hakuna kingine," alisema Savula.

Raila alimpokea rasmi Savula kwa vuguvugu la Azimio La Umoja ambalo hivi karibuni linadokezwa kuwa chama cha kisiasa mara tu marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa yatakapoidhinishwa na Bunge na kutiwa saini na Rais kuwa sheria

(Utafsiri: Samuel Maina)